• HABARI MPYA

  Tuesday, June 13, 2017

  TANZANIA HATARINI KUFUNGIWA NA FIFA

  Na Freddy Mapunda, DAR ES SALAAM
  TANZANIA iko hatarini kufungiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) baada ya kile kinachoonekana Serikali kutaka kuingilia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Jana TFF ilitoa taarifa ya mchakato wa uchaguzi wake, ambao imepanga ufanyike Agosti 12 mwaka huu mjini Dodoma, lakini leo Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lilio chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo limesimamisha zoezi hilo.
  Taarifa ya BMT iliyosainiwa na Katibu Mkuu wake, Mohammed Kiganja imesema kwamba TFF wameanza taratibu za uchaguzi bila kulitaarifu baraza hilo, hivyo mchakato huo ni ubatili na unasitishwa mara moja.
  “Vilabu, vyama na Mashirikisho ya Michezo yameundwa chini ya Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Namba 12 ya mwaka 1967 na marekebisho Namba 6 ya mwaka 1971 pamoja na kanuni za Usajili Namba 442 za mwaka 1999.
  Mshambuliaji wa U-17 ya Tanzania, Kevin Nashon Naftari akimtoka Habibou Soufiane wa Niger katika mechi ya mwisho ya Kundi B Fainali za U-17 mjini Port Gentil, Gabon
  Kwa kuwa mnaelekea kwenye uchaguzi mkuu, taratibu za uchaguzi wa viongozi zimefafanuliwa kwenye sera ya maendeleo ya Michezo Ibara ya 5:2:2,”imesema taarifa ya Kiganja kwenda kwa Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa leo.

  Kiganja amesema kwa mujibu wa kanuni za BMT, zilizotungwa chini ya kifungu cha 28 za mwaka 1999 kifungu namba 4, 6 (e), uwepo wa Kamati ya Nidhamu, Usuluhishi na Rufaa ibara ya 6 (9) (11) na B vinajieleza wazi juu ya majukumu ya Kamati hiyo.  
  Amesema kwa kuwa Tanzania inaongozwa kwa sharia na taratibu ilizojiwekea yenyewe, hivyo hakuna chama, klabu wala shirikisho lenye mamlaka ya juu ya BMT yenye nguvu ya kusimamia chaguzi za vyama.
  Kwa sababu hiyo, Kiganja amesimamisha zoezi hilo la uchaguzi wa TFF na kuwaita viongozi wa shirikisho hilo chini ya Rais wake, Jamal Malinzi katika kikao maalum kitakachofanyika ofisi za BMT, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Julai 1, mwaka huu kujadili pamoja na kupanga taratibu za uchaguzi huo.

  Inawezekana BMT ikawa inafanya hivyo kwa nia nzuri, lakini kutokana na FIFA chini ya Rais wake mpya, Gianni Infantino kuendelea kutilia mkazo sheria ya Serikali kutoingilia vyama na mashirikisho ya soka, Tanzania inajiweka matatani dhidi ya bodi hiyo ya mpira ya dunia.
  Machi mwaka huu, FIFA ya Mtaliano Infantino ilizifungia timu za Mali kushiriki michuano yote ya kimataifa baada ya Serikali yake kuingilia uendeshwaji wa shirikisho la soka la nchi hiyo.
  Mali ikaondolewa kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 nchini Gabon, kabla ya serikali ya nchi hiyo kubatilisha mpango wake na timu yao ikarejeshwa kwenye michuano hiyo na kufanikiwa kutwaa Kombe kwa mara ya pili mfululizo Mei mwaka huu. 
  Mali ilipatwa na adhabu hiyo baada ya Wizara yake ya Michezo kuwaondoa madarakani viongozi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo (FEMAFOOT).
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TANZANIA HATARINI KUFUNGIWA NA FIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top