• HABARI MPYA

    Wednesday, June 07, 2017

    STARS YAREJEA LEO, MECHI NA LESOTHO KUCHEZWA USIKU DAR

    Na Alfred Lucas, CAIRO
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania maarufu kwa jina la Taifa Stars, inatarajiwa kurejea Dar es Salaam leo kutoka Misri ambako iliweka iliweka kambi ya wiki kujiandaa na mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 dhidi ya Lesotho Juni 10, Uwanja.
    Taifa Stars wanatarajiwa kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Saa 6.30 mchana wa leo.
    Timu hiyo iliyosafiri kwa ndege wa Ethiopia, ilikuwa jijini Alexandria - Kaskazini kabisa mwa nchi ya Misri ambako ilipiga kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho unaotarajiwa kufanyika Jumamosi Juni 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Akizungumza mara baada ya mazoezi ya jana asubuhi, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amesema kwamba kimsingi amefanikiwa katika kile alichopangilia kukifanya akiwa Misri.
    “Kwanza kabisa niweze kumshukuru Mungu. Tulisafiri salama na kufanya mazoezi kwa siku saba hapa Misri. Na leo jioni tunanza safari ya kuelekea Cairo kwa ajili ya safari ya kurudi nyumbani. Naam, kambi ilianza tarehe 23 mwezi uliopita pale Dar es Salaam na tukaja kuendelea huku Misri.
    “Naweza kusema kuwa nimefanikiwa au tumefanikiwa. Kambi ni nzuri, mazingira ya kambi ni mazuri na tulifika mahali ambako hakuna mtu anayeweza kufanya movement (mizunguko) zozote za kutoka au kuingia kirahisi kwa sababu tulikuwa kwenye kambi ya Hoteli ya Nyota Tano, lakini ni Jeshi.
    “Mazoezi ya kawaida ya kiufundi napo tumefanya vema kwa maana wana vitu vyote tunavyohitaji vilipatikana hasa kufanya mazoezi usiku kwa sababu mchezo wetu utakuwa usiku. Nawaomba tu Watanzania waje kuiunga mkono timu yao,” amesema Mayanga.
    Naye, Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Himid Mao Mkami, amesema kwamba kambi ilikuwa nzuri yenye mafanikio ambayo matunda yake yatakuja kuonekana katika michezo mbalimbali ya kimataifa ukiwamo wa Jumamosi dhidi ya Lesotho.
    Mchezo huo dhidi ya Lesotho umepangwa kuanza Saa 2:00 usiku Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za AFCON za mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon.
    Mbali ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni Uganda na Cape Verde ambao pia wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa katika mchezo wa kwanza pia kuwania nafasi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS YAREJEA LEO, MECHI NA LESOTHO KUCHEZWA USIKU DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top