• HABARI MPYA

  Saturday, June 10, 2017

  STARS YAANZA VIBAYA MBIO ZA AFCON 2019, SARE 1-1 NA LESOTHO

  Na Shekha Jamal, DAR ES SALAAM
  TANZANIA imeanza vibaya mbio za kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Lesotho usiku wa leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa Kundi L.
  Sare hiyo inamaanisha kocha Salum Mayanga ameshindwa kuvunja mwiko wa muda mrefu wa Taifa Stars kutoshinda mechi zaidi ya mbili, baada ya kushinda mechi mbili za kirafiki mwezi Machi 2-0 dhidi ya Botswana na 2-1 dhidi ya Burundi.
  Katika mchezo wa leo, Tanzania ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 27 kupitia kwa Nahodha wake, Mbwana Ally Samatta kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya beki wa kushoto, Gardiel Michael kuangushwa nje ya boksi. 
  Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta (kushoto) akipiga shuti pembeni ya Thapelo Mokhele (kulia)

  Beki wa Taifa Stars,  Shomary Kapombe (kushoto) akipambana na Jane Thaba - Ntso wa Lesotho (kulia) 

  Winga wa Taifa Stars, Simon Msuva akipiga mpira mbele ya mabeki wa Lesotho

  Winga wa Taifa Stars, Shiza Kichuya akimpita beki wa Lesotho, Mafa Moremoholo  
  Hata hivyo, bao hilo halikudumu, kwani Lesotho, au Mamba walisawazisha dakika ya 34 kupitia kwa Thapelo Tale aliyeunganisha pasi nzuri ya Jane Thaba-Ntso.
  Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, timu zote zilishambuliana kwa zamu, lakini Lesotho ndiyo waliocheza vizuri zaidi kwa kuonana na kutawala sehemu ya kiungo.
  Na hiyo ilitokana na mfumo wa wenyeji kuweka mawinga wawili pembeni na washambuliaji wawili mbele, hivyo kujikuta inaelemewa sehemu ya katikati ya Uwanja ambako walikuwepo Himid Mao na Muzamil Yassin pekee.
  Lesotho ilipata pigo dakika ya 40 baada ya mfungaji wa bao lake, Tale kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo hivyo kocha Moses Maliehea akamuingiza Motebang Sera.
  Himid Mao alimsetia pasi nzuri Samatta dakika ya 49, lakini mpira wa kichwa aliopiga ukapaa juu ya lango na dakika ya 66, Thomas Ulimwengu naye nusura aipatia bao Stars kama si shuti lake kutoka nje baada ya krosi ya Shiza Kichuya.
  Kasi ya mashambulizi ya Stars iliongezeka mwishoni mwa mchezo baada ya mabadiliko yaliyofanywa mfululizo na Mayanga akiwatoa Thomas Ulimwengu, Simon Msuva na Muzamil Yassin na kuwaingiza Farid Mussa, Mbaraka Yussuf na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
  Nahodha Samatta hakucheza vizuri kipindi cha pili kutokana na kuonekana kukerwa na namna wachezaji wa Lesotho walivyokuwa wakimdhibiti watatu kwa mkupuo, lakini Mayanga akamuacha amalize mchezo.   
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Abdi Banda, Salim Mbonde, Himid Mao, Simon Msuva/Farid Mussa dk71, Muzamil Yassin/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dk71, Thomas Ulimwengu, Mbwana/Mbaraka Yussuf dk78, Samatta na Shiza Kichuya.
  Lesotho; Likano Mphuti, Mafa Moremoholo, Bokang Sello, Kopano Seka, Thapelo Mokhelo, Bokang Mothoana, Tumelo Khutlang/Mabuti Potloane dk61, Tsoanelo Koetle, Taphelo Talle, Hlompho Kaleko na Jane Thaba Ntso.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: STARS YAANZA VIBAYA MBIO ZA AFCON 2019, SARE 1-1 NA LESOTHO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top