• HABARI MPYA

    Tuesday, June 13, 2017

    SIMBA SC YAMTAMBULISHA ‘MTOA ROHO’ JOHN BOCCO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imemtambulisha mshambuliaji wake mpya, John Raphael Bocco ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Wekundu hao wa Msimbazi akitokea Azam FC.
    Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva leo amemkabdhi jezi ya klabu hiyo nahodha wa zamani wa Azam FC, kufutaia kukamilisha taratibu za kujiunga na timu hiyo kongwe nchini.
    Bocco, kama wachezaji wengine wa Azam wanaokwenda Simba, kipa Aishi Manula na beki Shomary Kapombe inafuatia kutofikia makubaliano ya kuongeza mikataba Azam FC.
    Rais wa Simba SC, Evans Aveva (kushoto), akimkabdhi jezi ya klabu hiyo mchezaji mpya, John Bocco kutoka Azam FC 

    Kwa kuwa Simba imefanikiwa kurejea kwenye michuano ya Afrika mwakani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 na ipo kwenye harakati za kuboresha kikosi, imeona ni vyema kutoa fedha kusajili nyota wa kiwango cha juu, akiwemo mfungaji huyo bora wa zamani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Na baada ya kusaini mkataba huo, Bocco ambaye ataendelea kulipwa Sh. Milioni 4 alizokuwa analipwa Azam FC, ameingia kwenye mazoezi makali ya kujiweka fiti zaidi ili akaweze kukabiliana na changamoto ya ushindani wa namba dhidi ya washambuliaji hatari wa Simba, Muivory Coast, Frederick Blagnon, Mrundi Laudit Mavugo na mzalendo, Juma Luizio.
    Kitu kimoja kizuri, Bocco anakwenda timu ambayo inafundishwa na kocha wake wa zamani, Mcameroon Joseph Marius Omog ambaye amewahi kufanya naye kazi Azam FC.
    Ikumbukwe, Bocco alijiunga na Azam FC mwaka 2007 akitokea Cosmopolitan ya Dar es Salaam na akaisaidia timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake kupanda Ligi Kuu mwaka 2008 akiibuka mfungaji bora wa Daraja la Kwanza.
    Baada ya hapo, Bocco akawa mshambuliaji tegemeo wa Azam FC akiiongoza kutwaa mataji kadhaa, ikiwemo Ligi Kuu mwaka 2014 na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, au Kombe la Kagame mwaka 2015.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAMTAMBULISHA ‘MTOA ROHO’ JOHN BOCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top