• HABARI MPYA

  Sunday, June 11, 2017

  MABINGWA WAPIGWA NYUMBANI UFUNGUZI KUFUZU AFCON 2019

  TIMU za Guinea, Msumbiji na Afrika Kusini zimepata ushindi wa ugenini katika mechi za ufunguzi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Cameroon 2019 jana.
  Guinea iliwaangusha mabingwa wa 2015, Ivory Coast mjini Bouake, Msumbiji ikawafunga mabingwa wa 2012, Zambia mjini Ndola na mabao ya kipindi cha pili ya Tokelo Rantie na Percy Tau yakapa Afrika Kusini ushindi wa kwanza kabisa dhidi ya Nigeria, mabingwa wa 2013 kwenye mechi ya mashindano.
  Mauritania pia imeshinda ugenini 1-0 dhidi ya Botswana, sawa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliyowafunga jirani zao, Kongo 3-1 wakati Burkina Faso, washindi wa tatu wa fainali za mwaka huu Gabon, wakapata ushindi kama huo pia dhidi ya Angola.

  Jean Michael Seri (kulia) na Franck Kessie wa Ivory Coast (kushoto) wakigombea mpira na Seydouba Soumah (katikati) wa Guinea jana

  Timu za Cameroon, Burundi, Guinea Bissau, Malawi, Mali na Sierra Leone zilishinda nyumbani, wakati mechi kati ya Cape Verde na Uganda ilisogezwa mbele kwa saa 24 baada ya wageni kuchelewa kufika.
  Seydou Doumbia alirejea kwenye kikosi cha Ivory Coast na kufunga mabao mawili, lakini Guinea mara mbili ilitoka nyuma kupata ushindi 3-2 huku nyota wa Bundesliga, Naby Keita akifunga bao la ushindi zikiwa zimesalia dakika 11.
  Lilikuwa ni pigo kwa kocha mpya wa Ivory Coast, Marc Wilmots, Mbelgiji ambaye mwaka jana alikuwepo kwenye michuano ya Euro, akitoka kufungwa 5-0 na Uholanzi Jumapili iliyopita katika mchezo wa kirafiki.
  Timu zote zilimuenzi kiungo wa zamani wa Ivory Coast, Cheikh Tiote, aaliyefariki dunia baaada ya kuzimia mazoezini na klabu yake ya China Jumatatu.
  Msumbiji imefungwa mechi 14 na kutoa sare nne katika mechi zao zilizopita na jirani zao, Zambia lakini mzaliwa wa Ujerumani, Stanley Ratifio mchezaji wa ridhaa wa timu ya wachezaji wa akiba wa FC Cologne, akiichezea Mambas mechi yake ya pili alifunga la dakika za mwishoni kufuta uteja huo.
  Afrika Kusini ilimpa mwanzo mzuri kocha kutoka England, Stuart Baxter aliyerejea kufundisha timu hiyo kwa mara ya pili baada ya kuifunga Nigeria Uyo.

  MATOKEO KAMILI MECHI ZA JANA
  Juni 10, 2017
  Tanzania 1-1 Lesotho
  Senegal 3 - 0 Equatorial Guinea
  Mali 2 - 1 Gabon
  Burkina Faso 3 - 1 Angola
  Ivory Coast 2 - 3 Guinea
  DRC 3 - 1 Kongo
  Sierra Leone 2 - 1 Kenya
  Guinea-Bissau 1 - 0 Namibia
  Nigeria 0 - 2 Afrika Kusini
  Niger 0 - 0 Swaziland
  Cameroon 1 - 0 Morocco
  Botswana 0 - 1 Mauritania
  Zambia 0 - 1 Msumbiji
  Burundi 3 - 0 Sudan Kusini
  Malawi 1 - 0 Comoro
  Libya 5 - 1 Shelisheli
  Juni 9, 2017
  Sudan 1 - 3 Madagascar
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MABINGWA WAPIGWA NYUMBANI UFUNGUZI KUFUZU AFCON 2019 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top