• HABARI MPYA

  Saturday, June 10, 2017

  KIPRE TCHETCHE ‘AZIFUNGIA VIOO’ SIMBA NA YANGA, ASAINI MALAYSIA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Muivory Coast, Kipre Herman Tchetche anayetakiwa na zote, Simba na Yanga amesaini mkataba wa miezi sita kujiunga na Terengganu City FC ya Malaysia akitokea Al Suwaiq ya Oman.
  Akizungunza na Bin Zubeiry Sports – Online usiku huu kwa simu kutoka Kuala Terengganu, Terengganu nchini Malaysia, Tchetche amesema kwamba ameondoka Suwaiq yenye maskani yake mji wa Salalah, Oman baadaa ya kumaliza mkataba.
  Kipre Tchetche akiwa ameshika skafu baada ya kusaini mkataba na picha ya chini akiwa na Kocha wa timu yake mpya

  Hata hivyo, Kipre amesema kwamba pamoja na kupata mkataba mzuri Terengganu City FC, lakini hakusaini muda mrefu kwa kuwa timu yenyewe ipo Daraja la Pili Malaysia.
  “Nimesaini mkataba mzuri ili niisadie timu hii kupanda, na wao wamevutiwa na mimi baada ya kuona kazi yangu Oman. Ni matarajio yangu nitaisaidia hii timu,”amesema. 
  Tchetche anaondoka Suwaiq baada ya kuiwezesha timu hiyo ya mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na Simba, Thuwein Ally kutwaa Kombe la Mfalme lijulikanalo kama Sultan Cup kwa ushindi wa 2-0 huku yeye akifunga mabao yote dhidi ya Dhofar FC Uwanja wa Sultan Qaboos Sport Complex mjini Muscat, Oman.
  Ikumbukwe mchezaji huyo alikwenda Oman akitokea Azam FC ya Tanzania aliyoichezea tangu mwaka 2011 alipojiunga nayo kutoka kwao Ivory Coast kabla ya kuuzwa kwa dola za Kimarekani 50, 000 zaidi ya Sh. Milioni 100 za Tanzania.
  Lakini awali, Tchetche, mwenyewe alisaini Al-Nahda Al-Buraimi pia ya Ligi Kuu pia ya Oman, ambayo ndiyo ilimtoa Azam FC akiwa amebakiza Mkataba wa mwaka mmoja.
  Licha ya Al Nahda kumalizana na Kipre Tchetche, lakini kwa kushindwa kulipa dola 50,000 za kuvunja Mkataba wa mchezaji huyo na Azam FC ilikuwa sababu tosha ya kumshuhudia akicheza sehemu nyingine ncini humo. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIPRE TCHETCHE ‘AZIFUNGIA VIOO’ SIMBA NA YANGA, ASAINI MALAYSIA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top