• HABARI MPYA

    Tuesday, June 06, 2017

    JOHN BOCCO ‘ADEBAYOR’ NI MCHEZAJI MPYA WA SIMBA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI John Raphael Bocco amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Simba SC, maana yake anahitimisha miaka yake 10 ya kuichezea Azam FC.
    Habari ziso na punje ya shaka ambazo Bin Zubeiry Sports – Online imezipata kutoka Simba SC, zinasema kwamba yapata wiki mbili sasa tangu Bocco, maarufu kwa jina la utani kama Adebayor asaini Msimbazi.
    Na kusaini kwa Bocco Simba kulifuatia kutofikia makubaliano ya mkataba mpya na timu iliyompatia umaarufu katika medani ya soka nchini, Azam FC.
    Bocco alitaka dau la Sh. Milioni 40 kusaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kucheza Azam FC kwa mshahara ule ule wa Sh. Milioni 4, lakini uongozi chini ya Meneja, Abdul Mohammed haukukubaliana naye.
    John Bocco amehitimisha miaka yake 10 ya kuichezea Azam FC kwa kusaini Simba SC

    Azam ilikuwa tayari kuendelea kumlipa Sh. Milioni 4 Bocco, lakini katika upande wa dau la usajili alitakiwa kuchukua Sh. Milioni 10 na mchezaji huyo akakataa.  
    Kwa kuwa Simba imefanikiwa kurejea kwenye michuano ya Afrika mwakani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 na ipo kwenye harakati za kuboresha kikosi, ikaona ni vyema kutoa Sh. Milioni 40 kumsajili mfungaji huyo bora wa zamani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Na baada ya kusaini mkataba huo, Bocco ambaye ataendelea kulipwa Sh. Milioni 4, ameingia kwenye mazoezi makali ya kujiweka fiti zaidi ili akaweze kukabiliana na changamoto ya ushindani wa namba dhidi ya washambuliaji hatari wa Simba, Muivory Coast, Frederick Blagnon, Mrundi Laudit Mavugo na mzalendo, Juma Luizio.
    Kitu kimoja kizuri, Bocco anakwenda timu ambayo inafundishwa na kocha wake wa zamani, Mcameroon Joseph Marius Omog ambaye amewahi kufanya naye kazi Azam FC.
    Ikumbukwe, Bocco alijiunga na Azam FC mwaka 2007 akitokea Cosmopolitan ya Dar es Salaam na akaisaidia timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake kupanda Ligi Kuu mwaka 2008 akiibuka mfungaji bora wa Daraja la Kwanza.
    Baada ya hapo, Bocco akawa mshambuliaji tegemeo wa Azam FC akiiongoza kutwaa mataji kadhaa, ikiwemo Ligi Kuu mwaka 2014 na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, au Kombe la Kagame mwaka 2015.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JOHN BOCCO ‘ADEBAYOR’ NI MCHEZAJI MPYA WA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top