• HABARI MPYA

  Sunday, June 11, 2017

  GOR MAHIA MABINGWA SPORTPESA SUPER CUP 2017, WAITWANGA AFC LEOPARDS 3-0 SHAMBA LA BIBI

  Na Shekha Jamal, DAR ES SALAAM
  GOR Mahia ya Kenya ndiye bingwa wa kwanza wa michuano mipya ya SportPesa Super Cup baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya mahasimu wao wa Kenya, AFC Leopards jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Ingwe wamezawadiwa kitita cha dola za Kimarekani 30,000 na pia watacheza na Everton ya England Julai 13 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, Gor wakaanza ‘kuiharibu sura’ Leopards kipindi cha pili kwa mabao mfululizo, wafungaji Timoth Otieno, Oliver Moloba na John Ndirangu.
  Otieno alifunga bao la kwanza dakika ya 60 kwa shuti akimalizia pasi ya mfungaji bora wa mashindano haya, Meddie Kagere, kabla ya Moloba kufunga la pili dakika ya 76 akimalizia pasi ya George ‘Blackberry’ Odhiambo na Ndirangu akafunga la tatu dakika ya 90 baada ya kupokea pasi ya Kenneth Muguna.
  Gor Mahia wakifurahia na Kombe lao baada ya kukabidhiwa leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam
  Ushindi huu pia unamaanisha Gor imeendeleza ubabe katika Mashemeji Derby, baada ya Jumapili ya Mei 7, mwaka huu Uwanja wa Nyayo mjini Nairobi, Kenya kushinda pia 3-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Kenya.
  Timoth Otieno alifunga pia siku hiyo dakika ya 83 bao la tatu, wakati mengine yalifungwa na Meddie Kagere dakika ya 18 na Odhiambo Blackberry dakika ya 35.
  Michuano hii iliyoanza Juni 5, ilishirikisha timu nane, nyingine Nakuru All Stars, Tusker FC za Kenya pia, Jang’ombe Boys ya Kenya, Yanga, Simba za Dar es Salaam na Singida United ya Singida.
  Yanga ni timu pekee ya Tanzania iliyofika Nusu Fainali na kutolewa kwa mikwaju ya penalti 4-2 na AFC Leopards baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
  Jang’ombe Boys ililambwa 2-0 na Gor Mahia katika mchezo wa kwanza, wakati Singida ilitolewa kwa penalti 5-4 na Leopards na Simba ilitupwa nje kwa penalti 5-4 na Nakuru All Stars. Michuano hiyo mwakani itafanyika Kenya.
  Kikosi cha Gor Mahia kilikuwa; Fredrick Odhiambo, Haroun Shakava, Innocent Wafula/John Ndirangu dk84, Wellington Ochieng, Joach Onyango, Philemon Otieno, Francis Kahata, Kenneth Muguna, Timothy Otieno, Meddie Kagere na George ‘Blackberry’ Odhiambo/Amos Nondidk84.
  AFC Leopards; Dennis Shikai, Otieno Timoth/Oliver Maloba dk73, Marcus Abwao, Joshua Mawira, Salim Abdallah, Duncan Otieno, Bernard Mangoli, Allan Kateregga, Vincent Oburu, Yakubu Ramadhani na Gilbert Fiamenyo.                        
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: GOR MAHIA MABINGWA SPORTPESA SUPER CUP 2017, WAITWANGA AFC LEOPARDS 3-0 SHAMBA LA BIBI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top