• HABARI MPYA

    Friday, June 09, 2017

    FAINALI SPORTPESA SUPER CUP 2017; LEOPARDS KULIPA KISASI KWA GOR J’PILI?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KWA mara ya kwanza, mahasimu wa jadi katika soka ya Kenya, Gor Mahia na AFC Leopards watakutana katika ardhi ya Tanzania Jumapili katika fainali ya michuano mipya kabisa, SportPesa Super Cup.
    Mchezo huo unatarajiwa kufanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni na ni baada ya Leopards maarufu kama Ingwe kuitoa Yanga ya Tanzania kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika ya 90 na Gor Mahia kuifunga 2-0 Nakuru All Stars ya Kenya pia.
    Yanga imethibitisha ni bingwa kweli wa Tanzania na ni timu bora hapa nchini baada ya kuwa mwenyeji pekee aliyefika Nusu Fainali, kufuatia, Singida United, Simba SC na Jang’ombe zote kutolewa na Wakenya katika Raundi ya kwanza tu.
    Atafunga tena? Meddie Kagere alifunga Mei 7 Uwanja wa Nyayo Gor Mahia wakiilaza AFC 3-0 katika Ligi ya Kenya

    Mamia ya mashabiki wa timu hizo zenye mvuto wa kipekee Kenya wanatarajiwa kusafiri kutoka sehemu mbalimbali nchini humo kuja kushuhudia fainali hiyo tamu nay a kihistoria Jumapili Uwanja wa Uhuru.
    Na kwa hapa nyumbani, tayari mashabiki wa timu pinzani za hapa wamegawana timu za kusapoti Jumapili, Yanga wakiichagua Gor Mahia inayotumia jezi za kijani na Simba wakiichagua Leopards (Chui) inayotumia jina la mnyama kama wao, lakini pia inavaa jezi nyekundu.
    Dhahiri patapendeza Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ikiandika historia ya kuwa Jiji la kwanza la Afrika Mashariki kuhodhi mechi ya mahasimu wa Kenya nje ya nyumbani kwao.
    Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Kenya Jumapili ya Mei 7, mwaka huu Uwanja wa Nyayo mjini Nairobi, Kenya.
    Na siku hiyo, Gor Mahia wakaibuka washindi wa ‘Derby’ ya kwanza ya msimu ya Mashemeji kwa kuilaza AFC Leopards 3-0, mabao ya Meddie Kagere dakika ya 18, George ‘Blackberry’ Odhiambo dakika ya 35 na Timothy Otieno dakika ya 83.
    Siku hiyo kikosi kilichoanza cha AFC Leopards kilikuwa; Ian Otieno, Joshua Mawira, Robinson Kamura, Samuel Ndung’u, Abdalla Salim, Duncan Otieno, Bernard Mang’oli, Allan Kateregga, Whyvonne Isuza, Paul Kiongera na Gilbert Fiamenyo.
    Katika benchi walikuwepo Gabriel Andika, Marcus Abwao, Yakubu Ramadhan, Mike Kibwage, Andrew Tololwa, Haron Nyakha na Marcellus Ingotsi
    Gor Mahia: Boniface Oluoch, Karim Nizigiyimana, Wellington Ochieng, Musa Mohammed, Haron Shakava, Kenneth Muguna, Ernest Wendo, Godfrey Walusimbi, George Odhiambo, Timothy Otieno na Meddie Kagere
    Benchi; Shaban Odhoji, Innocent Wafula, Philemon Otieno, Francis Kahata, Jean-Baptiste Mugiraneza, John Ndirangu and Jacques Tuyisenge.
    Sasa Mashemeji wanakutana katika mechi ya pili msimu huu nje ya Kenya, huku AFC Leopards wakiwa na kumbukumbu ya kulambwa 3-0 Mei 7 Nyayo.
    Swali ni je, Ingwe iko tayari kulipa kisasi kwa K’Ogalo Jumapili ‘Shamba la Bibi’? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona. Ila SportPesa Super Cup fainali ‘Derby ya Mashemeji’ si ya kukosa Jumapili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FAINALI SPORTPESA SUPER CUP 2017; LEOPARDS KULIPA KISASI KWA GOR J’PILI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top