• HABARI MPYA

  Monday, June 05, 2017

  DIDA AIPELEKA YANGA NUSU FAINALI SPORTPESA SUPER CUP

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup kufuatia ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Tusker ya Kenya, baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Kipa namba moja wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ alipangua vizuri penalti ya Clifford Alwanga kabla ya Stephen Owusu kugongesha mwamba wa juu mkwaju wake kukamilisha matuta mawili waliyopoteza Tusker.
  Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alikwenda kufunga penalti ya kwanza na wenzame wengine watatu, Mzambia Obrey Chirwa, Maka Edward Mwakalukwa na Said Mussa wakafunga pia, wakati waliofunga matuta ya Tusker ni Noah Wafula na Brian Osumba pekee.
  Yanga sasa itakutana na AFC Leopards ya Kenya pia katika Nusu Fainali Juni 8 Uwanja wa Uhuru kuwania kuingia fainali ya michuano ambayo bingwa atajinyakulia kitita cha dola za Kimarekani 30,000, zaidi ya Sh. Milioni 65 za Tanzania.
  Wachezaji wa Yanga wakiwa wamembeba kipa wao, Deogratius Munishi ‘Dida’ baada ya kupangua penalti na kuipeleka timu hiyo Nusu Faniali ya michuano ya SportPesa Super Cup

  Katika mchezo wa leo, Kocha Juma Mwambusi anayeiongoza timu hiyo badala ya bosi wake, George Lwandamina kwenda likizo kwao, Zambia alipanga wachezaji wengi wa timu ya vijana kutokana na wachezaji wengi wa timu ya kwanza kuwa kwenye timu zao za taifa.
  Na wachezaji hao wa Yanga B wakacheza vizuri na kufanikiwa kuwang’oa mabingwa wa Kenya katika hatua ya kwanza tu ya mashindano.
  Kivutio zaidi alikuwa ni kinda, Mussa Said aliyekuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kilichoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON U-17) mwezi uliopita nchini Gambia.
  Mchezaji huyo aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Emmanuel Martin na kwenda kuinogesha safu ya ushambuliaji ya Yanga kiasi cha kushangiliwa mno kwa ufundi wake na kujiamini kwake.
  Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mohammed Ally, Andrew Vincent ‘Dante’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Pato Ngonyani, Yussuf Mhilu, Maka Edward, Obrey Chirwa, Juma Mahadhi/Samuel Greyson dk81 na Emmanuel Martin/Mussa Said dk60.
  Tusker FC; Duncan Ochieng, Shivachi Collins, Martin Kiiza/Stephen Owusu dk64, Lloyd Wahonce, James Situma, Moses Ndawula/ Noah Wafula dk56, Anthony Ndolo/Brian Osumba dk86, Humphrey Mieno, Michael Khamati/Alwanga Cliford dk56, Allan Wanga na Hassan Abdul.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: DIDA AIPELEKA YANGA NUSU FAINALI SPORTPESA SUPER CUP Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top