• HABARI MPYA

    Wednesday, June 07, 2017

    CHANJI: SIHUSIKI NA USAJILI YANGA, MIMI NILIJIUZULU SIKU NYINGI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Isaac Chanji amekataa tetesi kwamba amerejea kwenye Kamati hiyo.
    Baadhi ya vyombo vya Habari nchini vimekuwa vikiripoti kwamba, Chanji pamoja na waliokuwa Wajumbe wenzake kwenye Kamati hiyo, Abdallah Ahmed Bin Kleb, Seif Ahmed ‘Magari’ na Mussa Katabaro wamerejea. Tayari Bin Kleb na Seif Magari nao wamekana kurejea kwenye Kamati hiyo.
    Kwa taarifa hizo, Chanji amesema kwamba amekuwa akipigiwa simu na wanachama wa Yanga kumshauri wachezaji wa kusajili, wakati hilo si jukumu lake.

    Mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Isaac Chanji (kushoto) akiwa na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa klabu kwa muda mfupi, Mfaransa Jerome Dufourg Desemba 29, mwaka jana Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati wa mchezo dhidi ya Ndanda 

    “Nimekuwa nikisumbuliwa sana na wanachama na wapenzi, wakinipigia mimi simu wakati mwingine wanataka kuniletea hadi wachezaji niwasajili wakati mimi hilo si jukumu langu na ni siku nyingi sipo kwenye hiyo Kamati,”amesema Chanji akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo.
    Chanji amesema kwamba yeye alijiuzulu tangu mwezi Juni, mwaka jana kwa sababu za kubanwa na majukumu yake ya kazi Serikalini.
    “Sasa hivi mimi nimebaki mwanachama kama wanachama wengine, nami pia kama nina ushauri au msaada wangu wowote nauwasilisha kwa uongozi, chini ya kaimu Mwenyekiti wetu, Isaac Chanji,”amesema.
    Chanji amesema kwamba yeye kama mpenzi na mwanachama wa Yanga pamoja na kuondoka kwenye Kamati na uongozi kwa ujumla, lakini mara chache amekuwa akijitikeza kusaidia.
    “Ninapofuata nafasi nimekuwa nakwenda kuwajulia hali wachezaji, nakwenda uwanjani kuangalia mechi, na wakati mwingine kuhamasisha, lakini haimaanishi nimerudi, hapana,”alisema.  
    Chanji aliondoka Yanga baada ya kuiwezesha kuingia kwenye mechi za Kundi A Kombe la Shirikisho, ikitoka kumaliza msimu vizuri kwa kuiwezesha pia timu kushinda mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
    Na sasa mwaka mmoja tu tangu Chanji aondoke, Yanga imesindwa kurudi hatua ya makundi ya michuano ya Afrika huku pia ikipokonywa mataji ta Ngao na ASFC na kufanikiwa kutetea la Ligi Kuu tu, tena kwa mbinde, ikiwazidi tu kwa wastani wa mabao mahasimu, Simba baada ya kulingana kwa pointi 68 kila timu baada ya mechi zote 30.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHANJI: SIHUSIKI NA USAJILI YANGA, MIMI NILIJIUZULU SIKU NYINGI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top