• HABARI MPYA

  Sunday, June 11, 2017

  AZAM FC YAMSAJILI KIPA WA MBAO MIAKA MIWILI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imemrejesha kipa wake wa zamani, Benedict Haule kwa kuingia naye mkataba wa miaka miwili.
  Azam FC inamsajili kipa huyo wa Mbao FC baada ya aliyekuwa kipa wake wa kwanza kwa misimu mitatu iliyopita, Aishi Manula kusaini Simba SC.
  Huyo anakuwa mchezaji wa pili Azam FC inamchukua kutoka Mbao FC ndani ya wiki moja, baada ya katikati ya wiki kumsajili kiungo Salmin Hoza kwa mkataba wa miaka miwili.
  Na kwa ujumla anakuwa mchezaji wa nne mpya kusajiliwa na timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, baada ya washambuliaji Waziri Junior kutoka Toto Africans ya Mwanza pia, Mbaraka Yussuf kutoka Kagera Sugar na Hoza.
  Ben Haule alidaka vizuri mechi za mwisho za msimu na kuinusuru Mbao FC kushuka Daraja, huku pia akiifikisha fainali ya ASFC
  Meneja wa Azam FC, Abdul Mohammed (kulia) akimkabidhi jezi ya klabu Ben Haule baada ya kusaini mkataba na chini wakati anasaini

  Haule ni kipa aliyeibukia timu ya vijana ya Azam FC kabla ya kuachwa kutokana na kuzidiwa uwezo na makipa wenzake wa wakati huo.
  Lakini kipa huyo hakukata tamaa, akaenda kujibidiisha na kupandisha kiwango chake kabla ya kusajiliwa Mbao FC iliyopanda Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
  Alisajiliwa kama kipa wa pili wa Mbao FC, lakini baada ya aliyekuwa kipa wa kwanza, Erick Ngwengwe kufungwa mabao rahisi matatu ndani ya dakika 10 za mwisho katika mchezo wa Ligi Kuu, Simba ikitoka nyuma kwa 2-0 na kushinda 3-2 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Aprili 10, mwaka huu aliondolewa kwenye timu na Ben Haule akaanza kudaka.
  Alifanikiwa kumalizia msimu vizuri akiiwezesha Mbao kubaki Ligi Kuu na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), ambako walifungwa na Simba 2-1 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
  Na baada ya kazi hiyo nzuri, malipo yake ndiyo anasaini mkataba wa mshahara mzuri kurejea nyumbani, Chamazi, Dar es Salaam.
  Haule sasa anakwenda kukutana tena na Metacha Boniphace Mnata aliyekuwa naye Azam akademi kuwania kulinda lango la klabu ya Chamazi kwa pamoja na mkongwe, Mwadini Ali.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAMSAJILI KIPA WA MBAO MIAKA MIWILI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top