• HABARI MPYA

    Friday, June 09, 2017

    AZAM FC YAIPA PIGO LINGINE YANGA, YAMSAJILI MBARAKA YUSSUF

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    AZAM FC imeipa pigo lingine Yanga SC baada ya kufanikiwa kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbaraka Yussuf Abeid kutoka Kagera Sugar ya Bukoba.
    Mbaraka amesaini leo asubuhi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam baada ya mazoezi ya timu ya taifa, Taifa Stars ambayo kesho inamenyana na Lesotho uwanjani hapo katika mechi ya Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
    Na mchezaji huyo aliyekuwa anawania pia na Yanga, amesaini mbele ya Meneja Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohammed na Meneja wa timu, Philipo Alando.
    Huyo ni mchezaji wa pili Azam FC wanaizidi kete Yanga, baada ya awali Waziri Junior kutoka Toto Africans kwenda hadi makao makuu ya klabu hiyo Jangwani na kupiga picha na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Salum Mkemi na kushikishwa Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu, lakini kesho yake akaenda kusaini timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake. 
    Mbaraka Yussuf akitia dole gumba kwenye fomu za Azam FC baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili. Kulia ni Meneja wa klabu, Abdul Mohammed na kushoto ni Meneja wa timu, Philipo Alando 

    Mchezaji huyo aliyeibukia timu ya vijana ya Simba, alishika nafasi ya pili kwa ufungaji wa mabao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, akifunga mara 12 na kuzidiwa bao moja na wote, Simon Msuva wa Yanga na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting waliofungana na kubeba pamoja kiatu cha dhahabu.
    Lakini katika sherehe za kuhitimisha msimu wa VPL, Mbaraka akatunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Ligi Kuu akiwaangusha Shaaban Iddi wa Azam FC na Mohammed Issa ‘Banka’ wa Mtibwa Sugar.   
    Mfungaji huyo wa bao la ushindi la Taifa Stars, ikiilaza 2-1 Burundi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Machi 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, alizaliwa Septemba 2 mwaka 1997, Kinondoni, Dar es Salaam na akasoma Shule ya Msingi Kumbukumbu na baadaye sekondari ya Tabata kabla ya kuhamia Kinondoni Muslim alikohitimu Kidato cha Nne.
    Mbaraka Yussuf Abeid (kulia) akiwatoka wachezaji wa Simba katika mechi ya Ligi Kuu msimu uliopita Bukoba
    Kinondoni Muslim ndiko haswa alikoanzia kucheza soka hadi mwaka 2014 alipokwenda kujiunga na timu ya vijana ya Simba SC ambako alicheza hadi 2015 akapandishwa timu ya kwanza chini ya kocha Muingereza, Dylan Kerr lakini wakati Ligi Kuu inakaribia kuanza akatolewa kwa mkopo Kagera Sugar. 
    Baada ya kumaliza mkataba wake wa mkopo wa mwaka mmoja, Mbaraka akasaini mkataba wa kujiunga na timu hiyo moja kwa moja ambako msimu huu amemaliza na anachukuliwa na Azam FC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAIPA PIGO LINGINE YANGA, YAMSAJILI MBARAKA YUSSUF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top