• HABARI MPYA

  Sunday, May 21, 2017

  TFF INAPASWA KUJITATHMINI NA KUANZA KUCHUKUA HATUA SASA

  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imefikia tamati jana, huku Yanga wakifanikiwa kutetea taji lao kwa mara ya pili mfululizo, hivyo kulibeba moja kwa moja baada ya kulitwaa mara tatu mfululizo. 
  Simba SC imemaliza nafasi ya pili kwa kuzidiwa tu wastani wa mabao na Yanga baada ya wote kuvuna pointi 68 katika mechi 30 za msimu.
  Bahati mbaya kwao, JKT Ruvu, Toto Africans na African Lyon zimeipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu, zikizipisha Mji Njombe, Lipuli ya Iringa na Singida United.
  JKT Ruvu imeshuka kwa mara ya kwanza tangu ilipopanda mwaka 2000 wakati kwa Toto na Lyon imekuwa desturi sasa kwao kupanda na kushuka.
  Ligi imemaliza, kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi bingwa amekwishapatikana, lakini bado kuna wasiwasi mkubwa tu wa matokeo kupinduliwa na bingwa akapatikana mezani.
  Hiyo inafuatia Simba kupeleka malalamiko Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) dhidi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kudai wapewe pointi tatu walizopokonywa.
  Nakala iliyosainiwa na Katibu wa Simba, Hamisi Kisiwa inaonyesha barua hiyo ilitumwa Mei 17 kwa njia ya Fax na nakala yake wakapewa TFF.
  Madai ya msingi ya Simba ni kurejeshewa pointi tatu walizopewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, maarufu kama Kamati ya Saa 72 baada ya kuikatia rufaa Kagera Sugar kwa madai ya kumtumia beki Mohammed Fakhi akiwa anatumia adhabu ya kadi za tatu njano.
  Simba SC ilifungwa 2-1 katika mchezo huo uliofanyika Aprili 2, mwaka huu Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, lakini Kamati ya Saa 72 ikawpa pointi tatu za mezani. Hata hivyo, Kagera Sugar wakakata rufaa TFF wakisema mchezaji wao hakuwa ana kadi tatu, bali mbili na wakarejeshewa pointi zao.
  Simba nao sasa wameamua kusonga mbele hadi FIFA ili warejeshewe pointi zao na hatimaye kutimiza ndoto zao za kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012.      
  Mara ya mwisho bingwa wa Ligi Kuu kupatikana mezani ilikuwa mwaka 2000, waathirika wakiwa Yanga, ambao baada ya kumaliza juu ya msimamo kwa matokeo ya uwanjani, Waziri wa Michezo wakati huo, Juma Kapuya akawapa pointi za mezani Mibwa Sugar na wakatwaa Kombe.
  Simba nao wanataka kuikumbusha Yanga machungu ya mwaka 2000, iwapo watashinda kesi yao FIFA.
  Inasikitisha baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu, tunashindwa kuanza kufikiria kutokea hapo, badala yake tunarudi nyuma kusubiri kujua tena nani atakuwa bingwa.
  Ukweli ni kwamba katika dunia ya leo kupitisha makosa madogo madogo kama hayo ambayo yanafanya sasa tusubiri majibu ya FIFA ili kumjua bingwa.
  Na makosa ya aina hii yanapita kwa sababu kuna watu pale Bodi ya Ligi na TFF hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.
  Na bahati nzuri kwao, Shirikisho liko chini ya Rais mpole, Jamal Malinzi ambaye sana ukisikia kamchukulia mtu hatua kamuhamisha idara, labda kutoka TFF kwenda Bodi.
  Lakini kumbe Malinzi hajui tu – anapaswa kuwachukuliwa watu hatua, ili iwe fundisho kwao wasirudie na kwa wengine wasifanye hivyo.
  Wakati tunasubiri majibu ya FIFA kuhusu malalamiko ya Simba, vyema Malinzi na wenzake katika Kamati ya Utendaji ya TFF wakafanya tathmini yao msimu na kuchukua hatua ili msimu ujao tuwe na Ligi nzuri zaidi.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF INAPASWA KUJITATHMINI NA KUANZA KUCHUKUA HATUA SASA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top