• HABARI MPYA

  Saturday, May 20, 2017

  SIMBA NA YANGA ZAMALIZA LIGI KUU NA POINTI SAWA, TOTO, LYON ZASHUKA DARAJA

  MATOKEO MECHI ZA MWISHO LIGI KUU LEO
  Simba SC 2-1 Mwadui FC
  Mbao 1-0 Yanga SC
  Azam 0-1 Kagera Sugar
  Stand 2-1 Ruvu Shooting 
  Prisons 0-0 African Lyon
  Ndanda 2-0 JKT Ruvu
  Majimaji 2-1 Mbeya City
  Mtibwa Sugar 3-1 Toto Africans

  Shiza Kichuya akipiga penalti kuifungia bao la kwanza Simba SC leo dhidi ya Mwadui FC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  PAZIA la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara limefungwa leo kwa vigogo, Simba na Yanga kumaliza na pointi sawa, 68 kila moja baada ya mechi 30.
  Hiyo inafuatia Simba kuibuka na ushinid wa 2-1 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Yanga wakichapwa 1-0 na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  Kwa matokeo hayo, Yanga inafanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu kwa wastani wake mzuri wa mabao, ingawa bado kuna tishio la Simba kwenda Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) mjini Zurich, Uswisi kudai pointi tatu za chee walizopokonywa baada ya kupewa kimakosa kufuatia kufungwa na Kagera Sugar.
  Baada ya kufungwa 2-1 na Kagera Sugar Aprili 2, mwaka Uwanja wa Kaitaba, Simba walimkatia rufaa beki Mohammed Fakhi na wakapewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi ikawa pointi tatu, kabla ya Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi na Wachezaji kuwapokonya pointi hizo kufatia Kagera Sugar kukata rufaa pia. 
  Mjini Mwanza, katika mchezo huo uliochezeshwa na Ludovick Charles wa Tabora aliyesaidiwa na washuika vibendera Makame Mdogo wa Shinyanga na Vincent Mlabu wa Morogoro, bao pekee la Mbao FC limefungwa na Habib Hajji dakika ya 23.
  Mjini Dar es Salaam dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika Simba ikiwa inaongoza 2-1 Uwanja wa Taifa, mabao yake yakifungwa na winga Shizza Ramadhani Kichuya na mshambuliaji Ibrahim Hajib Migomba, huku la Mwadui likifungwa na Paul Nonga.
  Kichuya alianza kufunga dakika ya 17 kwa mkwaju wa penalti baada yeye mwenyewe kuchezewa rafu na kipa wa Mwadui, Shaaban Hassan Kado.  
  Na kabla Mwadui hawajakaa sawa, Hajib akawatandika bao la pili dakika ya 24 akimalizia pasi ya Juma Luzio Ndanda. Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Nonga akaifungia Mwadui dakika ya 42 akimalizia krosi ya Hassan Kabunda.
  Matokeo ya mechi nyingin Kagera Sugar imeifunga Azam 1-0 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Stand United imeilaza 2-1 Ruvu Shooting Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Prisons imelazimishwa sare ya 0-0 na African Lyon Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Ndanda FC imeshinda 2-0 dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Mtibwa Sugar imeshinda 3-1 dhidi ya Toto Africans Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Majimaji imeshinda 2-1 dhidi ya Mbeya City Uwanja Maji Maji Songea.
  Hiyo inamaanisha, JKT Ruvu, Toto Africans na African Lyon ndizo zinaipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu, zikizipisha Mji Njombe, Lipuli ya Iringa na Singida United zilizopanda kutoka Daraja la Kwanza.
  Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa: Agyei Daniel, Janvier Bukungu, Mohammed Hussein, James Kotei, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Yassin Mzamiru, Loudity 
  Mavugo/Mwinyi Kazimoto dk53, Ibrahim Ajibu na Juma Luizio/Said Ndemla dk46.
  Mwadui: FC Shaaban Hassan, David Luhende, Nassor Hemed, Abdallah Mfuko, Joram Mgeveke, Razack Khalfan, Awadh Juma, Miraj Athumani, Salim Kabunda/Abdallah Seseme dk61, Hassan Kabunda na Paul Nonga.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA NA YANGA ZAMALIZA LIGI KUU NA POINTI SAWA, TOTO, LYON ZASHUKA DARAJA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top