• HABARI MPYA

    Tuesday, May 16, 2017

    SIMBA, MO DEWJI AMANI TENA, SASA NGUVU MOJA MWADUI NA MBAO WAFE

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    HATIMAYE harufu mbaya iliyotaka kuchafua hali ya hewa Msimbazi, imetoweka baada ya uongozi wa klabu ya Simba kumaliza tofauti zake na mfadhili wake, Mohammed ‘Mo’ Dewji.
    Hiyo inafuatia kikao maalum kilichofanyika mjini Dar es Salaam kutafuta suluhu ya tofauti zilizojitokeza baada ya uongozi wa Simba kuingia mkataba wa udhamini na kampuni ya SportPesa bila kumshirikisha Mo Dewji. 
    Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema leo jioni mjini Dar es Salaam kwamba Kamati ya Utendaji ya klabu imekutana na Mo Dewji na kufikia suluhisho zuri la kuendelea kuwa pamoja na pia kuukumbatia udhamini wa SportPesa.
    Amani tena; Kutoka kulia Rais wa Simba, Evans Aveva, Mo Dewji na Kaburu

    “Katika kikao hicho suala la changamoto ya mkataba wa SportPesa na masuala mengine yalijadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi. Tunapenda kuwaarifu wanachama na wapenzi wetu wa Simba SC kuwa tofauti zote zilizoonekana siku chache zilizopita zimezikwa rasmi,”amesema Kaburu. 
    Nyange amesema kwamba sasa uongozi wa klabu na mfadhili wao, Mo Dewji ni kitu kimoja tena na wanaunganisha nguvu zao kupambana washinde mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mwadui FC wiki ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Mbao FC mei 27 Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
    Dewji anayetaka kununua hisa Simba, alikasirishwa na uongozi wa klabu hiyo kwa kuingia mkataba wa udhamini na kampuni ya SportPesa bila kumshirikisha.na akataka alipwe fedha zake, Sh Bilioni 1.4 alizokuwa anaikopesha Simba kwa kulipa mishahara ya wachezaji na benchi la Ufundi, Sh Milioni 80 kila mwezi.
    Ikumbukwe Mo alikubaliana na uongozi wa Simba kununua asilimia 51 ya hisa kwa Sh. Bilioni 20 mara baada ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba utakapokamilika. Na katika makubaliano ya msingi baina yake na uongozi ni kwamba ikitokea kampuni inataka kuidhamini klabu ashirikishwe, jambo ambalo halikufanyika.
    Mbali na Dewji, Zacharia Hans Poppe naye alijiuzulu Ujumbe wa Kamati ya Utendaji na uongozi wa Kamati ya Usajili na ya ujenzi wa Bunju Complex baada ya kuchukizwa na kutohusishwa katika mkataba wa udhamini wa kampuni ya SportPesa.
    Lakini jana Poppe alisema kufuatia kikao chake na uongozi wa Simba juzi usiku wamemaliza tofuti hizo na kufikia makubaliano ya kurudi kuzungumza na Mo Dewji wamalize utata uliopo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA, MO DEWJI AMANI TENA, SASA NGUVU MOJA MWADUI NA MBAO WAFE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top