• HABARI MPYA

  Saturday, May 13, 2017

  MWAKYEMBE AWAASA TFF KUTUMIA VIZURI FEDHA ZA UDHAMINI TAIFA STARS ILI WAVUTIE WAWEKEZAJI ZAIDI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ametoa wito kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutumia vizuri fedha za udhamini wa kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) ili kuvutia wadhamini wengine wadogo wadogo kuingia kuisaidia timu hiyo.
  Dk Mwakyembe aliyasema hayo jana akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ukumbi wa Kivukoni 4, hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam baada ya SBL kusaini mkataba wa miaka mitatu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wa kuidhamini timu ya taifa, Taifa Stars kwa kwa dau la Sh. Bilioni 2.1.
   Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati) akishuhudia Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (kulia) akibadilishana mikataba na Mkurugenzi wa Serengeti Breweries Limited (SBL), Helene Weesie (kushoto)

  Dk Mwakyembe alisemakwamba fedha hizo zikitumika vizuri zitawavutia wadhamini wengine kujitokeza kuwekeza katika timu ya taifa na soka ya Tanzania kwa ujumla.
  “Tafadhali, msaada tunaoupata lazima tuutumie vizuri, tunavyoutumia vizuri hata wadogo wengine huko wanavutiwa kuja nao kuwekeza kusaidia timu yetu ya taifa, na mimi nina matumaini makubwa sana, kwamba katika miaka hii mitatu mine mitano inayokuja Tanzania tutang’ara,”alisema.   
  Waziri Mwakyembe akampongeza na kumshukuruu pia Mkurugenzi Mkuu wa SBL, Helene Weesie kwa udhamini huo na pia kuonyesha nia ya kuidhamini na timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.
  Mapema akizungumza na Waandishi wa Habari, Helene Weesie alisema kwamba ni matumaini yao sasa soka ya Tanzania itarudi juu tena kwenye viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) baada ya SBL kurejea.
  Hii ni mara ya pili kwa SBL kuidhamini timu ya taifa baada ya kampuni hiyo kufanya hivyo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2008 hadi 2011.
  Helene Weesie alisema uamuzi wa kampuni hiyo wa kuidhamini timu ya taifa unatokana na sera ya SBL ya kusaidia kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali za kijamii ikiwemo michezo.
  “SBL inaona fahari kuidhamini timu yetu ya taifa kwa mara nyingine. Tumechukua hatua hiii kwa kuwa tunaelewa mchango wa sekta michezo katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Aidha tunaamini kuwa udhamini wetu utachangia kukuza vipaji vya vijana wetu pamoja na kuleta hamasa kubwa kwa mashabiki na wapenzi wa timu ya taifa,” alisema Weesie.
  Kwa upande wake, Rais wa TFF aliishukuru SBL kwa kukubali kuidhamini Taifa Stars jambo ambalo alisema litasaidia katika kufanikisha maandalizi mazuri na ushiriki kikamilifu wa timu hiyo katika mashindano mbalimbali, ndani nan je ya nchi.
   “Udhamini wa SBL umekuja kwa wakati mwafaka, wakati ambapo timu yetu ya taifa ipo katika hatua za  maandalizi kwa mashindano ya kikanda na kimataifa,” alisema Malinzi.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MWAKYEMBE AWAASA TFF KUTUMIA VIZURI FEDHA ZA UDHAMINI TAIFA STARS ILI WAVUTIE WAWEKEZAJI ZAIDI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top