• HABARI MPYA

    Saturday, May 20, 2017

    LIGI KUU YATIA NANGA LEO, KUNA WA KUIZUIA YANGA?

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MELI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliyoanza safari yake Jumamosi ya Agosti 20 mwaka jana, inatia nanga leo Mei 20, 2017.
    Mechi saba zitachezwa kwenye viwanja tofauti – kuanzia Taifa, Dar es Salaam ambako Simba SC watakuwa wenyeji wa Mwadui FC ya Shinyanga na CCM Kirumba mjini Mwanza, ambako mabingwa watetezi, Yanga watakuwa wageni wa Mbao FC.
    Mechi nyingine ni kati ya Azam na Kagera Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Maji Maji na Mbeya City Uwanja wa Maji Maji, Songea, Stand United na Ruvu Shooting Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mtibwa Sugar na Toto Africans Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Tanzania Prisons na African Lyon Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Ndanda FC na JKT Ruvu Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
    Yanga inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 68, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 65, Azam FC 52, Kagera Sugar 50, Mtibwa Sugar 41, Ruvu Shooting 36, Stand United 35, sawa na Mwadui, Tanzania Prisons 34, Mbeya City 33, Maji Maji 32, African Lyon 31, Mbao FC 30, sawa na Ndanda FC, Toto African 29 na JKT Ruvu 23 baada ya kila timu kucheza mechi 29.
    Abiria wapya watatu wa MV Ligi Kuu, Singida United, Njombe Mji na Lipuli ya Iringa tayari wapo kwenye mlango wa kupandia meli hiyo na tiketi zao, wakati JKT Ruvu tayari safari yake imefikia tamati na baada ya mechi za leo timu mbili nyingine za kuteremka zitajulikana.
    Toto, Mbao, Ndanda, Maji Maji na African Lyon kati ya hizo kuna timu mbili za kuungana na JKT Ruvu – na hilo litajulikana baada ya mechi za leo jioni.  
    Yanga wamekwishaanza kushangilia ubingwa tangu baada ya mchezo dhidi ya Toto Africans wakishinda 1-0, lakini ili wawe na amani, wanatakiwa kushinda mchezo wa leo dhidi ya Mbao FC, ili kuwafunga mdomo mahasimu wao, Simba SC ambao wametishia kukata rufaa FIFA kutaka warudishiwe pointi tatu za mezani za Kagera Sugar.
    Simba wanaamini wakishinda kesho na Yanga wakafungwa na Mbao, wanaweza kutimiza ndoto za ubingwa kama watashinda na rufaa yao FIFA.  
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepeleka Kombe la mfano kwenye Uwanja wa Taifa na Kombe halisi Uwanja wa CCM Kirumba ili kati ya Simba na Yanga timu moja ikabidhiwe taji ikishinda ubingwa wa ligi.
    Sahau kuhusu mchuano wa ubingwa na vita ya kuepuka kushuka Daraja, uhondo mwingine katika mechi za leo za kufunga msimu ni kinyang’anyiro cha ufungaji bora wa Ligi Kuu, kikiwahusisha Simon Msuva wa Yanga mabao 14, Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting mabao 13 na Mbaraka Yussuf wa Kagera Sugar mabao 13.
    Wakati MV Ligi Kuu inakwenda kutia nanga leo jioni, maswali ni matatu, nani wa kuizuia Yanga kutetea ubingwa, nani mfungaji bora na timu zipi zinashuka?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LIGI KUU YATIA NANGA LEO, KUNA WA KUIZUIA YANGA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top