• HABARI MPYA

    Thursday, May 18, 2017

    KILA LA HERI SERENGETI BOYS LEO DHIDI YA ANGOLA

    Na Mwandishi Wetu, LIBREVILLE
    TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys leo inarejea Uwanja wa L’Amitie mjini Libreville kumenyana na Angola katika mchezo wake wa pili wa Kundi B Fainali za Vijana Afrika chini ya umri wa miaka 17 zinazeondelea mjini hapa.
    Serengeti Boys inayofundishwa na Bakari Nyundo Shime, anayesaidiwa sana na Mshauri wa Ufundi, Mdenmark Kim Poulsen itahitaji ushindi katika mchezo wa leo kuweka hai matumaini ya kusonga mbele baada ya kulazimisha sare ya 0-0 kwenye mchezo wa kwanza na Mali, ambayo leo itamenyana na Niger.
    Kwa ujumla timu zote za Kundi B zitakuwa zinasaka ushindi wa kwanza leo, baada ya Angola pia kutoka sare ya 2-2 na Niger kwenye mchezo wa kwanza.       
    Kundi A tayari Ghana imekuwa ya kwanza kutinga Nusu fainali baada ya kuwafunga wenyeji, Gabon mabao 5- 0 jana Uwanja wa Port Gentil. 
    Mshambuliaji na Nahodha, Eric Ayiah aliye katika kiwango kizuri na kiungo, Emmanuel Toku kila mmoja alifunga mabao mawili leo, wakati Patmos Arhin aliyetokea benchi kipindi cha pili alifunga linguine.
    Matokeo hayo yanamaanisha Ghana inafikisha pointi sita na mabao tisa baada ya Jumapili kushinda 4-0 dhidi ya Cameroon katika mchezo wake wa kwanza.
    Maana yake pia Ghana wamejikatia tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia za U-17 baadaye mwaka huu, wakati wenyeji wanapoteza nafasi ya kusonga mbele baada ya mechi ya kwanza kufunga pia 5-1 na Guinea.
    Mchezo uliotangulia wa Kundi A jana, Cameroon ilijiweka mguu nje baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Guinea. 
    Kwa matokeo hayo, Guinea inafikisha pointi nne baada ya awali kushinda 5-1 dhidi ya wenyeji Gabon, wakati Cameroon inaokota pointi ya kwanza kutokana na sare hiyo, baada ya awali kufungwa 4-0 na Ghana.
    Mshambuliaji wa Les Syli Cadets, Djibril Fandje Toure aliifungia bao la kuongoza Guinea dakika ya 22 ambalo linakuwa bao lake la nne kwenye mashindano haya, kabla ya Stephane Zobo kuisawazishia Cameroon dakika ya 67.
    Kila la heri Serengeti Boys ya Watanzania katika mchezo wa leo. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki timu yetu ya vijana ishinde leo. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI SERENGETI BOYS LEO DHIDI YA ANGOLA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top