• HABARI MPYA

    Tuesday, May 16, 2017

    KAMATI YA SAA 72 YAMFUNGIA REFA, YAMFUTIA KADI NYEKUNDU MBARAKA YUSSUF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, ijulikanayo kama Kamati ya Saa 72, iliketi mwishoni mwa wiki iliyopita na kupitia mchezo mmoja baada ya mwingine na kuibuka na uamuzi ufuatao.
    Mechi namba 212 (Yanga 2 Vs Kagera Sugar 1). Kamati imefuta kadi nyekundu ya moja kwa moja aliyopewa mchezaji Mbaraka Yussuf wa Kagera Sugar baada ya kubaini hakutenda kosa lililosababisha mwamuzi ampe adhabu hiyo. Uamuzi huo umefanywa kwa mujibu wa Kanuni ya 9(8) ya Ligi Kuu. 
    Pia Mwamuzi wa mechi hiyo, Ngole Mwangole ameondolewa kuchezesha Ligi Kuu ya Vodacom kwa vile uamuzi aliofanya haukuwa sahihi. Hatua dhidi ya Mwamuzi Mwangole imechukuliwa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1a) ya Ligi Kuu.
    Mbaraka Yussuf wa Kagera Sugar amefutiwa kadi nyekundu aliyoonyshwa kwenye mechi dhidi ya Yanga 

    Hii ni mara ya pili kwa Ngole kushindwa kutafsiri sheria uwanjani kwani katika duru la kwanza alionywa baada ya kukataa bao JKT Ruvu ilipocheza na Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu ya ismu huu wa 2016/17. 
    Mechi namba 214 (JKT Ruvu 2 Vs Azam 2). Klabu ya Azam FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kutoingia vyumbani, na badala yake kukaa nje. Kitendo hicho ni kwenda kinyume na Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu, na adhabu imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu. 
    Mechi namba 215 (Mbao FC 1 Vs Tanzania Prisons 0). Mchezaji Jeremiah Juma wa Tanzania Prisons amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga ngumi mpinzani wake. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu. 
    Pia timu ya Tanzania Prisons imeagizwa kurudisha mpira uliochukuliwa na mshabiki wake baada ya kumalizika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 16, 2017 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. 
    Msimamizi Msaidizi wa Kituo cha Mwanza aliripoti kwa Meneja wa Prisons, Bw. Enock Mwanguku tukio la shabiki huyo aliyechukua mpira huo na kuingia kwenye gari la timu hiyo. Meneja huyo aliahidi kufuatilia, lakini hadi timu yake inaondoka uwanjani hakutoa mrejesho wowote. 
    Mechi namba 220 (Majimaji 3 Vs Mwadui 0). Klabu ya Majimaji imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.
    Mechi namba 224 (Yanga 2 Vs Tanzania Prisons 0). Klabu zote zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kutoingia vyumbani na kusababisha wachezaji wakaguliwe wakiwa nje ya vyumba. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMATI YA SAA 72 YAMFUNGIA REFA, YAMFUTIA KADI NYEKUNDU MBARAKA YUSSUF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top