• HABARI MPYA

  Thursday, May 11, 2017

  FARID MUSSA TARATIBU NYOTA YANG’ARA HISPANIA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MAKOCHA wa timu ya vijana ya Deportivo Tenerife wamemuambia winga wa kimataifa wa Tanzania, Farid Mussa hana muda mrefu kabla ya kuanza kucheza Ligi kubwa Ulaya.
  Hiyo inafuatia makocha hao kuvutiwa na kiwango cha mchezaji huyo katika mechi zake za timu ya vijana DC Tenerife ya Hispania.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu leo kutoka Hispania, Farid amesema kwamba juzi baada ya kufunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao katika ushindi wa 5-1 Uwanja wa Heliodoro Rodriguez walimpongeza sana na kumuambia atafika mbali.
  Farid Mussa akiichezea timu ya vijana ya Deportivo Tenerife juzi Uwanja wa Heliodoro Rodríguez 

  “Juzi nilifunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao, baada ya mechi wakanifuata kwa furaha na kuniambia mimi ni mchezaji mkubwa wa baadaye, sina muda mrefu nitacheza ligi kubwa. Kwa kweli imenifariji sana na kunitia moto wa kujituma zaidi,”amesema Farid.
  Kwa wiki hii peke yake, Farid amefikisha mabao matatu baada ya Jumatatu kufunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao katika ushindi wa 3-0.
  Farid alijiunga na klabu hiyo ya Santa Cruz de Tenerife, Tenerife, visiwa vya Canary Desemba mwaka jana kwa mkopo wa muda mrefu wa msimu kutoka Azam FC ya Dar es Salaam. 
  Azam FC ilimtoa kwa mkopo Farid kwenda CD Tenerife kwa makubaliano maalum baada ya winga huyo kufuzu majaribio katika klabu hiyo Aprili mwaka jana alipokwenda na Mkurugenzi wa klabu yake, Yussuf Bakhresa.
  Farid alitua Hispania kwa mara ya kwanza Aprili 21, mwaka jana baada ya kuichezea Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance mjini Tunis, Tunisia ikifungwa 3-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda 2-1 Dar es Salaam.
  Na ilimchukua wiki moja tu Farid kuwakuna kwa kipaji chake makocha wa Tenerife na kutaka kumnunua, lakini Azam ikakataa na kuamua kumtoa kwa mkopo Desemba, 2016.
  Na baada ya kutua Tenerife akapangiwa kuanza kuchezea kikosi cha U-20 ili kupata uzoefu kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza kinachocheza Segunda, Ligi ya pili kwa ukubwa Hispania.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: FARID MUSSA TARATIBU NYOTA YANG’ARA HISPANIA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top