• HABARI MPYA

  Sunday, May 14, 2017

  DILI LA SPORTPESA LISIWAFANYE SIMBA WAKAJISAHAU; MPIRA HAUJICHEZI WENYEWE

  MIEZI kadhaa baada ya kuupoteza udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), neema mpya imeshuka mtaa wa Msimbazi, yalipo makao makuu ya klabu ya Simba.
  Hiyo ni baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano kudhaminiwa na kampuni ya SportPesa Tanzania.
  Katika mkataba huo uliosainiwa mjini Dar es Salaam Ijumaa, Simba watavuna Sh. Bilioni 4.96 katika kipindi hicho cha miaka mitano.
  Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas alisema siku hiyo kwamba wameingia mkataba huo kwa dhumuni la kuendeleza soka nchini na kuisaidia klabu ya Simba kufikia malengo yake.
  Akifafanua, Tarimba ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa mahasimu wa Simba, Yanga alisema kwamba, katika mkataba huo, mwaka wa kwanza watatoa Sh. Milioni 888 na miaka itakayofuata wataongeza asilimia 5 na miaka miwili ya mwisho watatoa Sh. Bilioni 1 na kwamba fedha hizo zitatolewa kwa awamu nne kwa mwaka.
  Pamoja na hayo, Tarimba akasema kwamba Simba watatakiwa kuyathibitisha matumizi ya fedha hizo kwamba yalifanyika kwa maendeleo ya soka.
  Alisema licha ya mkataba huo, pia kutakuwa na motisha klabu hiyo ikishinda mataji, mfano kwa ubingwa wa Ligi Kuu watapewa zawadi ya Sh. Milioni 100.
  Simba ikishinda Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame itazawadiwa pia na wakifanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika watapata Sh. Milioni. 250.
  Kwa upande wake, Rais wa Simba, Evance Elieza Aveva alisema kwamba mkataba huo utakuwa chachu kubwa ya kutimiza azma ya kufanya vizuri kwa klabu hiyo kuanzia sasa.
  Aveva anasema hayo wakati Simba ikiwa katika moja ya misimu mizuri kwao baada ya muda mrefu, kwani pamoja na kwamba bado wapo kwenye mbio za ubingwa, lakini pia wameingia kwenye fainali ya Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Simba wanakabana koo na mabingwa watetezi, Yanga katika kuwania ubingwa, wote wakiwa na pointi 65, lakini wapinzani wao kwa sasa wapo juu kwa mabao yao zaidi na wana mchezo mmoja zaidi.
  Na Simba watamenyana na Mbao FC katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Mei 28 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
  Simba watacheza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu na Mwadui FC wakati Yanga itacheza mechi zake mbili za mwisho dhidi ya timu za Mwanza, Toto Africans na Mbao FC.
  Bingwa wa Ligi Kuu atacheza Ligi ya Mabingwa na bingwa wa Kombe la ASFC atacheza Kombe la Shirikisho Afrika.
  Simba ilicheza michuano ya Afrika mara ya mwisho mwaka 2013 ilipotolewa Raundi ya Kwanza tu ya Ligi ya Mabingwa na Recreativo de Lobolo ya Angola, ikifungwa 1-0 Dar es Salaam na 
  4-0 Angola.
  Wazi Simba wana kiu siyo tu ya mataji bali kwanza kurudi kwenye michuano ya Afrika na hiyo ndiyo itakuwa njia nzuri ya kutoa asante kwa SportPesa kwa udhamini wao.
  Baada ya kukosa mataji yote na hata nafasi ya kucheza michuano ya Afrika msimu uliopita, Aveva alisema kwamba hali ngumu ya kifedha iliwafanya washindwe kushindana na Yanga na Azam.
  Imekuwa bahati kwao msimu huu, Yanga na Azam wote hawakuwa katika ubora wao na ndiyo maana Simba wameingia fainali ya Kombe la ASFC na Mbao FC na huku bado wapo kwenye mbio za ubingwa.
  Na sasa wana udhamini wa SportPesa maana yake hawana tatizo la kiuchumi tena na ndiyo tusema watafute kisingizio kingine iwapo hawatafanya vizuri.
  Dhahiri Simba wanatakiwa kujipanga vyema kumalizia msimu vizuri ili watimize malengo yao ya angalau kutwaa taji moja kubwa na pia kurejea kwenye michuano ya Afrika.
  Na hilo linawezekana iwapo viongozi wa Simba hawatalewa sifa kutokana na udhamini wa SportPesa na kuona sasa wamemaliza kazi na kusahau kwamba kumbe mpira haujichezi wenyewe. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: DILI LA SPORTPESA LISIWAFANYE SIMBA WAKAJISAHAU; MPIRA HAUJICHEZI WENYEWE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top