• HABARI MPYA

  Friday, May 19, 2017

  ABDUL SULEIMAN: MFUNGAJI WA BAO LA USHINDI SERENGETI BOYS ALIYECHEZA NA JERAHA KISOGONI

  Na Mahmoud Zubeiry, LIBREVILLE
  NDOTO za Tanzania kucheza Fainali za Kombe la Dunia za Vijana chini ya umri wa miaka 17 zinakaribia kutimia baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Angola kwenye mchezo wa Kundi B Fainali za Afrika jioni ya leo Uwanja wa L’Amittee mjini Libreville, Gabon.
  Shujaa wa Tanzania leo alikuwa ni kiungo mshambuliaji, Abdul Suleiman aliyefunga bao la ushindi dakika ya 69, akimalizia pasi ya Yohana Oscar Nkomola.
  Na baada ya Mali nayo kuifunga Niger 2-1 katika mchezo wa pili leo, sasa inalingana kwa pointi na Serengeti Boys na idadi ya mabao pia, ya kufunga na kufungwa. Pointi nne kila timu, mabao mawili ya kufunga na moja la kufungwa. 
  Kijana huyo aliyezaliwa mwaka 2001 ambaye alichukuliwa timu ya vijana kutoka Mtwara, alifunga bao hilo akiwa na mshono wa nyuzi tatu kichwani baada ya kuumia kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Mali Jumatatu.
  Abdul Suleiman akipatiwa huduma ya kwanza baada ya kuumia katika mchezo wa leo 
  Dk. Gilbert Kigadya akimhudumia Abdul Suleiman leo 
  Abdul Suleiman akinyoosha viungo kabla ya kuinuka kurejea uwanjani
  Abdul Suleiman (kulia) katika mchezo wa leo
  Abdul Suleiman katikati ya wachezaji wa Angola leo 
  Abdul Suleiman akiwa amebebwa kwenye machella na jeraha lake ameziba na plasta
  Abdul Suleiman akiwa mazoezini jana kujiandaa na mchezo wa leo

  Abdul Suleiman alishindwa kuendelea na mchezo na kumpisha Israel Mwenda dakika ya 72 baada ya kugongana na mchezaji wa Mali na kuchanika kisogoni kiasi cha kuvuja damu nyingi kabla ya kushonwa nyuzi tatu baadaye kambini, hoteli ya Nomad.
  Na akakosa mazoezi mepesi ya Jumanne, lakini jana akarudi kwenye mazoezi magumu ya nje ya viwanja vya L’Amittee kujiandaa na mchezo wa leo.
  Ni ushujaa wa hali ya juu aliounyesha Abdul kwa kukubali kushiriki mazoezi siku moja baada ya kushonwa nyuzi tatu, tena eneo la nyuma ya kichwa.
  Na hakika benchi la Ufundi la Serengeti Boys liliuona umuhimu wa mchezaji huyo hata wakaamua kumpanga kwenye mchezo wa leo.
  Pamoja na kufunga bao la ushindi, lakini kwa ujumla Abdul alicheza vizuri sana akianza kama kiungo wa kulia na baadaye kumaliza kama mshambuliaji wa pili.
  Kipindi cha kwanza alicheza kama kiungo wa pembeni kulia, lakini baada ya Kevin Nashon Naftali kwenda kucheza nafasi ya kiungo mchezeshaji kufuatia kutoka kwa Enrick Vitalis Nkosi, Abdul akaenda kucheza kama mshambuliaji wa pili na akaifungia bao hilo Serengeti.
  Na kuna wakati aliumia baada ya kugongana na wachezaji wa Angola, lakini akatibiwa na kurejea uwanjani kumalizia mchezo.
  Serengeti Boys sasa itasafiri hadi Port Gentil Jumapili kwa mchezo wa mwisho wa Kundi B, dhidi ya Niger wakihitaji sare tu ili kujihakikishia tiketi ya Kombe la Dunia la U-17 mwaka huu.
  Na hiyo inasababishwa na ushujaa wa Abdul Suleiman kucheza akiwa majeruhi na kwenda kuifungia bao la ushindi Serengeti Boys ikiilaza 2-1 Angola.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ABDUL SULEIMAN: MFUNGAJI WA BAO LA USHINDI SERENGETI BOYS ALIYECHEZA NA JERAHA KISOGONI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top