• HABARI MPYA

  Tuesday, April 04, 2017

  TRA ‘WAWASHUSHA KWENYE BASI’ SERENGETI BOYS WAKIWA WANAKWENDA KWA MAKAMU WA RAIS

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia kampuni ya udalali na minada ya Yono, wamekamata basi la timu ya taifa, ambalo kwa sasa linatumiwa na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys.
  Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online mchana huu kwamba basi limechukuliwa katika hoteli ya Urbun Rose, Kisutu, Dar es Salaam likiwa linawasubiri wachezaji wa Serengeti Boys liwapeleke kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu.
  Wachezaji wa Serengeti Boys wamealikwa nyumbani kwa Mama Samia kwenye hafla maalum ya kuagwa kabla ya safari ya Morocco kesho kwenda kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na fainali za U-17 Afrika nchini Gabon Mei mwakani.
  Hatua hii inakuwa kiasi cha wiki tatu baada ya TRA kupitia kampuni ya Udalali na Minada ya Yono kuzifunga ofisi za TFF kutokana na deni kubwa la kodi na la muda mrefu.
  Deni hilo linakubwa zaidi linatokana na kodi za mishahara ya aliyekuwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbrazil Maximo kwa miaka minne tangu 2016 hadi 2010.
  Deni lingine linalosababisha ofisi za TFF kufungwa ni la kodi ya Ongezeko la Thamani (VaT) la ziara ya timu ya taifa ya Brazil nchini mwaka 2010 ilipokuwa njiani kwenye Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Dunia.
  Mwesigwa amesema kwamba baada ya kufungwa kwa Ofisi wamekuwa wakiwasiliana na Karibu wa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, Profesa Ole Gabirel ili kukutana kutatua tatizo hilo, lakini kwa bahati mbaya hawajafanikiwa.
  “Inaonekana Katibu wa Wizara yuko bize, maana muda mrefu tunaomba kukutana naye kuzungumzia hili deni, kwa kuwa mdaiwa ni Wizara yake na Hazina, lakini waathirika ni sisi TFF,”amesema. 
  Serengeti Boys inatarajiwa kuondoka kesho Saa 10: 45 jioni kwa ndege ya Emirates kwenda Morocco kupitia Dubai, ambako watalala siku moja.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TRA ‘WAWASHUSHA KWENYE BASI’ SERENGETI BOYS WAKIWA WANAKWENDA KWA MAKAMU WA RAIS Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top