• HABARI MPYA

  Wednesday, April 05, 2017

  SAFARI NJEMA SERENGETI, TUNAWATAKIA MAANDALIZI MEMA

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha wachezaji 23 wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kimeondoka jioni ya leo kwenda Morocco kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo nchini Gabon kuanzia Mei 14 mwaka huu.
  Kikosi hicho kinachotumia ndege ya shirika la Emirates, itapitia Dubai ambako vijana hao watalala kabla ya kuendelea na safari kesho mapema.  
  Serengeti Boys imekuwa kambini tangu Januari 29, mwaka huu na katika kipindi hicho imepata mechi tatu za kujipima nguvu.
  Machi 30, 2017 ilicheza Burundi ‘Intamba Murugamba’ na kushinda mabao 3-0 kabla ya kurudiana tena Aprili 1, mwaka huu na kushinda mabao 2-0, mechi zote mbili zikipigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Ghana ‘Black Starlets’ Aprili 3 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Wachezaji wa Serengeti Boys wakiwa na Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere leo kabla ya sfaari yao ya Morocco 

  Serengeti Boys iliagwa rasmi jana na Makamu wa Rais, Mama Samia Hassan Suluhu nyumbani kwake, Oysterbay, Dar es Salaam katika hafla iliyodhuriwa pia na Waziri wa Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.
  Serengeti Boys itakuwa kambini mjini Rabat, Morocco kwa kambi ya mwezi mmoja kuanzia Aprili 5, mwaka huu na ikiwa huko itacheza pia mechi za kirafiki zisizopungua mbili dhidi ya wenyeji Morocco na ama Tunisia au Misri.
  Mei 1, mwaka huu Serengeti Boys itakwenda Younde, Cameroon kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya wenyeji Mei 3 na 6, mwaka huu kabla ya Mei 7 kwenda Gabon ambako Serengeti Boys imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.
  Kila la kheri Serengeti Boys. Tunawatakia maandalizi mema na tunawaomba Watanzania wenzetu kuendelea kuichangia timu hii kwa namba ya 223344 kutoka mitandao yote ya simu.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAFARI NJEMA SERENGETI, TUNAWATAKIA MAANDALIZI MEMA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top