• HABARI MPYA

    Monday, April 03, 2017

    MECKY MEXIME UKIPENDA MUITE KIBOKO YA VIGOGO

    Na Mahmoud Zubeiry, BUKOBA
    MAKOCHA watatu wa kigeni wa Simba, Mcameroon Joseph Omog, Mganda Jackson Mayanja na Mkenya Iddi Salim jana waliondoka kinyonge Uwanja wa Kaitaba, Bukoba baada ya dakika 90 na ushei za mpambano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar.
    Hiyo ilitokana na kipigo cha mabao 2-1 katika mchezo huo, ambao walihitaji pointi tatu ili kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, kufuatia mahasimu wao, Yanga kushinda 1-0 dhidi ya Azam Jumamosi.
    Lakini mabao ya Mbaraka Yussuf Abeid kipindi cha kwanza na Edward Christopher Shijja kipindi cha pili dhidi ya moja la Muzamil Yassin yaliwatotesha Uwanja wa Kaitaba.
    Mecky Mexime akiiongoza Kagera Sugar dhidi ya Simba jana Uwanja wa Kaitaba
    Timu iliyoshinda jana inafundishwa na kocha mzalendo, tena mwalimu chipukizi, Mecky Mexime Silili Kianga akisaidiwa na mchezaji mwenzake wa zamani wa Morogoro, Ally Jangalu.
    Jangalu alicheza Reli miaka ya 1990 na Mexime akaibuka mwishoni mwa miaka hiyo Mtibwa Sugar na kutamba miaka ya 2000.
    Sifa moja kubwa ya Mecky Mexime ni kujiamini na kuzungumza chochote anachokiamini bila kumuhofia mtu.
    Na kwa sababu kila sifa ina faida na hasara zake, naye Mexime wakati fulani kusema kwake ukweli kumewahi kumponza akapoteza nafasi ya timu ya ukocha Msaidizi timu ya taifa, Taifa Stars mwaka 2015 alipokuwa chini ya Mholanzi, Mart Nooij na nafasi yake kuchukuliwa na Mayanga. 
    Uzuri mmoja, tangu anacheza Mexime si mtu wa vinyongo – kuna wachezaji wana vinyongo hata wakichezewa rafu kwa bahati mbaya hawasamehi milele, lakini si Mecky.
    Yote tisa – kumi ni kazi yake nzuri uwanjani Mexime, Nahodha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars ambayo ndani ya muda mfupi imekwishampambanua kama mmoja wa makocha bora vijana na hazina ya taifa.
    Mexime akiwa amebebwa na wachezaji wake jana baada ya mechi
    Mexime akisalimiana na makocha watatu wa kigeni wa Simba, kutoka kulia Mayanja, Omog na Salim kabla ya mechi
    Anajua kutengeneza timu. Anawajua wachezaji. Anajua kufundisha. Ana nidhamu, ingawa inapobidi kusema ukweli huwa hajali athari zozote.
    Kuna wakati alianzisha kampeni ya kupiga vita wachezaji wa kigeni magalasa wanaosajiliwa nchini akiwaponda wengine hawawezi hata kuumiliki mpira vizuri. “Mchezaji ana-drible (anakokota) chumba kizima” lilikuwa neno maarufu kutamkwa na Mexime. 
    Na jeuri hiyo hutokana pia na matokeo yake mazuri ya uwanjani – akizifunga timu vigogo zenye walimu wa kigeni wanaolipwa fedha nyingi.
    Septemba mwaka 2014, Mexime aliiongoza Mtibwa Sugar kuifunga 2-0 Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiwa chini ya mwalimu, Mbrazil Marcio Maximo.
    Kuanzia mwaka 2006 hadi 2008 Maximo alikuwa kocha wa Taifa Sars, ambayo Mexime alikuwa beki na Nahodha.
    Na huo ndiyo ulikuwa mchezo uliopandisha heshima yake kama mwalimu, wakati huo akiwa anaanza anza kuwa Kocha Mkuu Mtibwa Sugar kufuatia kuondoka kwa Salum Mayanga aliyekuwa mkuu wake.
    Na jana kawafunga Simba wakiwa na kocha mkubwa, Mcameroon Omog hivyo kuendeleza rekodi yake ya ‘kuvitia’ mchanga vitumbua vya makocha wa kigeni. Alikuwa mwenye furaha sana, akiamini mwenyewe anazidi kujenga CV yake. Mecky Mexime, ukipenda muite kiboko ya vigogo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MECKY MEXIME UKIPENDA MUITE KIBOKO YA VIGOGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top