• HABARI MPYA

    Wednesday, April 05, 2017

    DK MWAKYEMBE ATOA SIKU MBILI TRA IMALIZAME NA TFF

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR E SALAAM
    WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harison Mwakyembe ametoa siku mbili mgogoro baina ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kushughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi ili uishe moja kwa moja.
    Dk Mwakyembe aliagiza hayo jana nyumbani kwa Makamu wa Rais, Mama Samia Hassan Suluhu, Oysterbay, Dar es Salaam wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wachezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys wanaokwenda Morocco leo kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na fainali za Afrika nchini Gabon mwezo ujao.
    Mwakyembe ameagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake akutane na Katibu wa Wizara ya Fedha na kwa pamoja wakakae na Kamishna Jenerali wa TRA ndani ya siku mbili wazungumze na kutatua tatizo hilo. 
    Waziri wa Michezo, Dk Harrison Mwakyembe (katikati) ametoa siku mbili TRA kumalizana na TFF
    “Ikishindikana hiki kikao kufanyika mheshimiwa (Mama Samia) nitakuja kushitaki kwako. Hicho kikao naomba kifanyike kama nilivyoagiza mapema, sitaki kusikia tena kuhusu hilo deni,”alisema Dk Mweakyembe jana na kuongeza;.
    “Ninaogopa nisipoyasema haya mapema (TRA), watakuja kukamata basi wakati linakwenda Uwanja wa Ndege tukachelewa ndege ya kwenda Morocco,”.
    Dk. Mwakyembe alisema anachukua hatua hiyo kwa sababu baada ya kulifuatilia deni lenyewe linaoikabili TFF linaonekana ni Serikali. 
    Kauli ya Dk Mwakyembe ilifuatia TRA kupitia kampuni ya udalali na minada ya Yono kukamata basi la timu ya taifa, Taifa Stars ambalo kwa sasa linatumiwa Serengeti Boys.
    Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa aliiambia Bin Zubeiry Sports – Online jana kwamba basi lilichukuliwa katika hoteli ya Urbun Rose, Kisutu, Dar es Salaam likiwa linawasubiri wachezaji wa Serengeti Boys liwapeleke kwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu
    Hatua hii inakuja kiasi cha wiki tatu baada ya TRA kupitia Yono pia kuzifunga ofisi za TFF kutokana na deni kubwa la kodi na la muda mrefu.
    Deni hilo la Sh. Bilioni 1.2 linatokana na kodi za mishahara ya waliokuwa makocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo na Mdenmark, Jan Borge Poulsen kuanzia mwaka mwaka 2016 hadi 2010.
    Tayari TFF chini ya Rais wake, Jamal Malinzi imefanikiwa kulipa deni lingine la zaidi ya Sh. Milioni 400 kodi ya Ongezeko la Thamani (VaT) la ziara ya timu ya taifa ya Brazil nchini mwaka 2010 ilipokuwa njiani kwenye Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Dunia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DK MWAKYEMBE ATOA SIKU MBILI TRA IMALIZAME NA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top