• HABARI MPYA

  Tuesday, April 04, 2017

  BENKI YA NMB YARIDHISHWA NA UDHAMINI WAKE AZAM FC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, jana asubuhi ilifanya ziara kwa wadhamini wake wakuu Benki ya NMB, ambayo imeonyesha kuridhishwa na udhamini wake kwa mabingwa hao. Azam FC imetumia ziara hiyo kujifunza mambo mbalimbali yaihusuyo benki hiyo inayoongoza nchini kwa sasa, ikiwemo kuwapelekea makombe matatu waliyopata kipindi cha udhamini wa NMB kuanzia msimu wa 2014-2015 ilipoanza hadi sasa.
  Akizungumza wakati wa kuikaribisha timu hiyo, Afisa Mkuu wa Fedha NMB, Waziri Barnabas, alisema kuwa wanayofuraha kubwa kuendelea na udhamini wao kwa Azam FC huku akiipongeza kwa mafanikio wanayoendelea kuyapata na kuwaomba waendelee kuongeza juhudi.
  “Leo sisi ni furaha kuwaona wachezaji wakiwa hapa, tunawapa hongera sana kwa mafanikio mnayoendelea kupata, na muendeleze juhudi tunatarajia makubwa kutoka kwa Azam na tunaona itakuja kuwa ni timu ambayo ni ya mfano Tanzania na Afrika kwa ujumla, kwa hiyo hongera mnayo sapoti yetu kwa ujumla, tunafuraha sana leo mmeweza kutuletea baadhi ya makombe ambayo mmepata na wafanyakazi wetu wamefurahi kuwa pamoja na nyie,”
  Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba akiongea kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC aliushukuru uongozi wa NMB kwa kuendelea na udhamini huo huku akidai kuwa kupitia ushirikiano wao wamefanikiwa kutimiza mambo mengi ya maendeleo ya timu hiyo.
   “Huu udhamini tunaouzungumza ni ushirikiano ambao umetusogeza sana na Azam FC na tunaamini kabisa kwamba baada ya muda mfupi watu wengine wanaweza kuuliza kwamba kwanini Azam FC na sio wengine? Lakini siri ni moja tu kutengeneza mfumo wako mzuri, kila kitu kiwe na uwazi, uwajibikaji uwe unaonekana, halafu baada ya hapo watu watakuja kufanya kazi na wewe,” alisema.
  Kwa mara ya kwanza NMB kuipa udhamini Azam FC ilikuwa ni mwanzo mwa msimu wa 2014/15 ukiwa ni wa miaka miwili baada ya kutwaa taji la kwanza la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) 2013/14 kwa rekodi ya kutopoteza mchezo wowote, udhamini ambao umeongezwa tena msimu huu.
  Wafanyakazi wa NMB walipata fursa ya kupiga picha za kumbukumbu wakiwa na makombe waliyoshinda Azam FC. Makombe ambayo Azam FC imechukua tangu kuanza kwa udhamini wa NMB, Taji la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) iliyolitwaa mwaka juzi, Ngao ya Jamii waliyoibeba mwaka jana, Kombe la Mapinduzi mwaka huu na lile taji la michuano ya Vijana ya Afrika Mashariki mwaka jana.
  Wachezaji walitia saini katika mpira ambao ulibaki kama kumbukumbu ya ujio wao hapa Makao makuu ya NMB jijini Dar Es Salaam.
  Wakati huo huo: Fainali ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017), kati ya Azam FC na Ndanda FC itafanyika kesho Aprili 5, 2017 saa 1.00 usiku kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, imefahamika.
  Kadhalika, Robo Fainali ya nne ya mwisho ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017), kati ya Young Africans na Tanzania Prisons FC itafanyika Aprili 22, 2017 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
  Tayari timu za Mbao FC ya Mwanza na Simba ya Dar es Salaam, zimefuzu kwa hatua ya Nusu Fainali.
  Mbao iliifunga Kagera Sugar mabao 2-1 katika mchezo ulifanyika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera Machi 18, 2017 ilihali Machi 19, mwaka huu Simba iliilaza Madini ya Arusha kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
  Bingwa wa michuano hi ambayo msimu huu ilishirikisha timu 86 ikiwa ni pamoja na za Ligi Kuu ya Vodacom (timu 16); Ligi Daraja la Kwanza (timu 24); Ligi Daraja la Pili (timu 24) na mabingwa wa mikoa timu 22, atawakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho - CAF.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BENKI YA NMB YARIDHISHWA NA UDHAMINI WAKE AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top