• HABARI MPYA

    Saturday, March 11, 2017

    YANGA YALAZIMISHWA SARE NA ZANACO, 1-1

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC wamelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Zanaco ya Zambia katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Matokeo yanamaanisha Yanga watahitaji ushindi wa ugenini katika mchezo wa marudiano nchini Zambia ili kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na maarefa kutoka Djibouti, Djamal Aden Abdi aliyeyesaidiwa na Hassan Yacin na Farhan Salime, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Wachezaji wa Yanga wakiwa wamezubaa baada ya Zanaco kusawazisha bao leo
    Winga wa Yanga, Simon Msuva akimiliki mpira mbele ya beki wa Zanaco
    Kiungo wa Yanga, Thabani Kamusoko akijivuta kupiga shuti mbele ya beki wa Zanaco
    Beki wa Yanga, Hassan Kessy akimtoka beki wa Zanaco 
    Winga wa Yanga, Emmanuel Martin akipiga shuti mbele ya beki wa Zanaco

    Bao hilo lilifungwa na winga machachari wa timu hiyo, Simon Happygod Msuva dakika ya 39 baada ya kuwachambua mabeki wa Zanaco kufuatia pasi nzuri ya kiungo Mzambia, Justin Zulu.
    Bao hilo lilikuja baada ya Yanga kubadilisha maarifa ya kuwashambulia Zanaco, kutoka kutumia mipira ya kutokea pembeni hadi kuamua kuingia ndani ya eneo la hatari kwa kugongeana pasi.
    Kwa dakika zote 30 za awali, Zanaco hawakuwa na kazi ngumu kudhibiti mashambulizi yatokeayo pembeni ya Yanga, lakini baada ya mabingwa wa Tanzania, kubadilika hali ikawa ngumu upande wake.
    Pamoja na kufunga bao moja, lakini ndani ya dakika 15 za kuelekea mwisho wa kipindi cha kwanza, Yanga walikosa mabao mawili zaidi ya wazi.
    Kipindi cha pili Zanaco walikuja na maarifa mapya na kufanikiwa kuziba mianya ya Yanga kupenyezeana pasi hivyo kupunguza kasi ya wawakilishi hao wa Tanzania.
    Yanga ikarudi kutumia mipira mirefu ya kutokea pembezoni mwa Uwanja kujaribu kulazimisha mashambulizi langoni mwa Zanaco, lakini safu ya ulinzi ya mabingwa hao wa Zambia ilikuwa imara.
    Hatimaye Zanaco wakafanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 78  kupitia kwa mshambuliaji wake Mghana, Attram Kwame aliyetumia mwanya wa mabeki wa Yanga kuzubaa kusubiri wapinzani wao watoe nje mpira kiungwana (Fair Play) baada ya mchezaji mwenzao, Obrey Chirwa kuangushwa.
    Kwame alifunga mbee ya mabeki wa kati watatu wa Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan na Vincent Bossou na kipa wao Deogratius Munishi ‘Dida’ baada ya krosi kutoka wingi ya kulia.
    Bao hilo lilionekana kabisa kuwavunja nguvu Yanga na kutoka hapo wakaanza kucheza ili kumalizia mchezo kwa sare na si kutafuta ushindi.
    Kikosi cha Yanga leo kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Mwinyi Hajji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Vincent Bossou, Kevin Yondan, Simon Msuva, Justin Zulu, Donald Ngoma/Emmanuel Martin dk58, Thabani kamusoko/Juma Mahadhi dk60 na Obrey Chirwa.
    Zanaco; Racha Kola, Ziyo Kola, Zimiseleni Moyo, Chongo Chirwa, Saith Sakala/Kennedy Musonda dk69, Taonga Mbwemya, Richard Kasonde, Attram Kwame, Augustine Mulenga, Ernest Mbewe/Ayoub Lyanga dk85 na George Chilufya.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YALAZIMISHWA SARE NA ZANACO, 1-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top