• HABARI MPYA

  Monday, March 06, 2017

  YANGA SASA HASIRA ZOTE KWA KILUVYA UNITED

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  YANGA SC inaelekeza nguvu zake katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kufuatia kuzidiwa kete na mahasimu wao, Simba katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Yanga jana ililazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji, Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro hivyo kushindwa kurejea kileleni mwa Ligi Kuu kutokana na kuendelea kuzidiwa pointi mbili na vinara, Simba SC.
  Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema leo kwamba baada ya timu kuwasili kutoka Morogoro, inakwenda moja kwa moja kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Kiluvya United kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Baada ya mchezo huo wa hatua ya 16 Bora Kombe la ASFC, Yanga itarudi kambini kujiandaa na mchezo wa kwanza wa hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika Machi 11 dhidi ya Zanaco FC ya Zambia Uwanja wa Taifa pia.
  “Timu itaendelea na mazoezi leo jioni kujiandaa na mchezo wa kombe la TFF dhidi Kiluvya benchi la Ufundi limesema pamoja na ratiba ngumu inayowakabili, lakini wapo tayari kupambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika michezo yote miwili,”amesema Mkwasa. 
  Na Mkwasa amewaomba wapenzi wa Yanga kujitokeza kwa wingi katika michezo yote miwili ili kuipa sapoti timu yao. 
  Timu saba tayari zimefuzu Robo fainali ya ASFC, wakiwemo washindi wa pili wa mwaka jana, Azam FC, Simba SC zote za Dar es Salaam, Ndanda FC ya Mtwara, Madini ya Arusha, Mbao FC ya Mwanza, Prisons ya Mbeya na Kagera Sugar.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SASA HASIRA ZOTE KWA KILUVYA UNITED Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top