• HABARI MPYA

  Sunday, March 12, 2017

  YANGA INAWEZA KUIFUNGA ZANACO KWAO, HAKUNA SHAKA KABISA

  MASHABIKI wa Yanga SC  jana waliondoka kinyonge Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya timu yao kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Zanaco ya Zambia katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Unyonge wao ulikuwa wa kujikatia tamaa, kwamba baada ya kulazimishwa sare nyumbani hawafikirii kama timu yao inaweza kufurukuta ugenini.
  Kwani matokeo hayo yanamaanisha Yanga watahitaji ushindi wa ugenini lazima katika mchezo wa marudiano nchini Zambia wiki ijayo ili kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na maarefa kutoka Djibouti, Djamal Aden Abdi aliyesaidiwa na Hassan Yacin na Farhan Salime, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na winga machachari wa timu hiyo, Simon Happygod Msuva dakika ya 39 baada ya kuwachambua mabeki wa Zanaco kufuatia pasi nzuri ya kiungo Mzambia, Justin Zulu.
  Bao hilo lilikuja baada ya Yanga kubadilisha maarifa ya kuwashambulia Zanaco, kutoka kutumia mipira ya kutokea pembeni hadi kuamua kuingia ndani ya eneo la hatari kwa kugongeana pasi.
  Kwa dakika zote 30 za awali, Zanaco hawakuwa na kazi ngumu kudhibiti mashambulizi yatokeayo pembeni ya Yanga, lakini baada ya mabingwa wa Tanzania, kubadilika hali ikawa ngumu upande wao.
  Pamoja na kufunga bao moja, lakini ndani ya dakika 15 za kuelekea mwisho wa kipindi cha kwanza, Yanga walikosa mabao mawili zaidi ya wazi.
  Kipindi cha pili Zanaco walikuja na maarifa mapya na kufanikiwa kuziba mianya ya Yanga kupenyezeana pasi hivyo kupungusa kasi ya wawakilishi hao wa Tanzania.
  Yanga ikarudi kutumia mipira mirefu ya kutokea pembezoni mwa Uwanja kujaribu kulazimisha mashambulizi langoni mwa Zanaco, lakini safu ya ulinzi ya mabingwa hao wa Zambia ilikuwa imara.
  Hatimaye Zanaco wakafanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 78  kupitia kwa mshambuliaji wake Mghana, Attram Kwame aliyetumia mwanya wa mabeki wa Yanga kuzubaa kusubiri wapinzani wao watoe nje mpira kiungwana (Fair Play) baada ya mchezaji mwenzao, Obrey Chirwa kuangushwa.
  Kwame alifunga mbele ya mabeki wa kati watatu wa Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan na Vincent Bossou na kipa wao Deogratius Munishi ‘Dida’ baada ya krosi kutoka wingi ya kulia.
  Bao hilo lilionekana kabisa kuwavunja nguvu Yanga na kutoka hapo wakaanza kucheza ili kumalizia mchezo kwa sare na si kutafuta ushindi.
  Na haikustaajabisha mashabiki wa Yanga waliotarajia ushindi wakiondoka kinyonge Uwanja wa Taifa jana.
  Lakini sikuona kwa sababu gani mashabiki wa Yanga wanaondoka kinyonge, ikiwa katika siku za karibuni timu yao imekuwa ikifanya vizuri zaidi mechi za ugenini kuliko za nyumbani kwenye mechi za Afrika.
  Katika hatua ya awali ya mchujo, Yanga iliitoa Ngaya Club de Mde ya Comoro kwa jumla ya mabao 6-2, lakini nyumbani ililazimishwa sare ya 1-1 ikitoka kushinda 5-1 Moroni.
  Hata mwaka jana, Yanga iliitoa APR ya Rwanda katika hatua kama hii ya 32 Bora, lakini nyumbani ililazimishwa sare baada ya kushinda 2-1 Kigali.
  Hata hiyo, Zanaco nayo inaonekana haina makali sana inapocheza nyumbani, kwani katika hatua ya awali ya mchujo ililazimishwa sare ya 0-0 na APR Lusaka kabla ya kwenda kushinda 1-0 Kigali.
  Mashabiki na wana Yanga kwa ujumla hawapaswi kuikatia tamaa timu yao, badala yake wakati benchi la Ufundi linaiandaa timu kwa mchezo wa marudiano na wao wajichange kwenda kuisapoti timu yao kwenye mchezo wa marudiano.
  Wazambia walikuja kwa wingi jana Uwanja wa Taifa, wengine wakazi wa hapa, wengine wamekuja na timu na wengine walikuwa hapa kwa biashara zao. 
  Lakini wakajipanga kuja Taifa kuisapoti timu yao. Na mashabiki wa Yanga waendeleze desturi yao ya kusafiri kwenda kuisapoti timu yao popote.
  Kiufundi jana Yanga iliathiriwa na kukosa washambuliaji pale mbele, kwani Ngoma alionekana kabisa kucheza kwa kujilazimisha au kulazimishwa akiwa na maumivu ya goti.
  Na mshambuliaji mwingine tegemeo wa timu hiyo, Amissi Tambwe naye pia ni majeruhi, wakati chipukizi Malimi Busungu na Matheo Anthony tunaweza kujiridhisha hawana faida tena katika timu.
  Nadhani umefika wakati badala ya kulazimisha majeruhi kucheza, ni bora Simon Msuva na Obrey Chirwa wachezeshwe kama washambuliaji wa kati na pembeni wachezeshwe hao akina Geoffrey Mwashiuya, Emmanuel Martin au Juma Mahadhi.
  Deus Kaseke anaweza kucheza nafasi yoyote ya kiungo cha ushambuliaji, kulia, kushoto na hata katikati – katika kipindi hiki kigumu huyu ni silaha muhimu kwa timu.
  Zaidi benchi la Ufundi la Yanga limeona makosa baada ya mchezo wa jana na sasa tunasubiri kuona wataitumiaje wiki hii kujiandaa kwa mchezo wa marudiano.
  Naamini Yanga inaweza kuifunga Zanaco kwao bila shaka kabisa na kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA INAWEZA KUIFUNGA ZANACO KWAO, HAKUNA SHAKA KABISA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top