• HABARI MPYA

  Sunday, March 19, 2017

  THOMAS ULIMWENGU KUTOJIUNGA NA TAIFA STARS SABABU HAYUKO FITI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa AFC Eskilstuna ya Ligi Kuu ya Sweden, Thomas Emmanuel Ulimwengu hataweza kujiunga na kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa ajili ya michezo ya kirafiki ya kimataifa wiki ijayo.
  Taifa Stars inaingia kambini leo Machi 19, 2017 kwenye Hoteli ya Urban Rose, Dar es Salaam na kikosi hicho cha kocha Salum Mayanga kitamkosa  Ulimwengu kwa kuwa hayuko fiti.
  Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema leo kwamba taarifa alizozipata kocha Mayanga kutoka Sweden ni kwamba Ulimwengu kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa madaktari wa timu hiyo ya AFC Eskilstuna. 
  Thomas Ulimwengu hataweza kujiunga na kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya michezo ya kirafiki ya kimataifa wiki ijayo

  Hivyo sasa Mayanga atabaki na washambuliaji Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Abdul-Rahman Mussa (Ruvu Shooting).
  Mbali ya hao, nyota wengine aliowataja Jumatatu iliyopita ni walinda milango, Aishi Manula (Azam FC), Deogratius Munishi (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
  Walinzi wa pembeni upande wa kulia aliwataja Shomari Kapombe (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba) na Gadiel Michael (Azam FC).
  Mayanga aliwataja walinzi wa kati Vicent Andrew (Yanga SC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Erasto Nyoni (Azam FC) ilihali aliwataja viungo wa kuzuia kuwa ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude (Simba SC).
  Kadhalika wako viungo wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC), Frank Domoyo (Azam FC) na Muzamil Yassin (Simba) wakati viungo wa kulia waliotajwa ni Simon Msuva (Yanga SC) na Shizza Kichuya (Simba SC).
  Viungo wa kushoto ni Farid Mussa (Teneriffe, Hispania) na Hassan Kabunda (Mwadui FC) wakati wasaidizi wake ni Kocha Wa Makipa, Patrick Mwangata; Meneja wa timu, Danny Msangi; Mtunza Vifaa, Ally Ruvu wakati Daktari wa timuatakuwa Richard Yomba huku Daktari wa viungo akiwa ni Gilbert Kigadya.
  Taifa Stars inatarajiwa kucheza na Botswana Machi 25, 2017 kabla ya kuivaa Burundi Machi 28, mwaka huu katika michezo kirafiki wakati huu wa Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: THOMAS ULIMWENGU KUTOJIUNGA NA TAIFA STARS SABABU HAYUKO FITI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top