• HABARI MPYA

    Thursday, March 16, 2017

    PLUIJM ATUA SINGIDA UNITED NA KUSAJILI ‘MIDO’ MZIMBABWE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    ALIYEKUWA kocha wa Yanga, Mholanzi Hans Van der Pluijm amejiunga na klabu ya Singinda United iliyopanda Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu ujao.
    Aliyefanikisha dili la Pluijm kujiunga na timu hiyo ya Singida ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo na Mbunge wa Singida, Mwigulu Nchemba ambaye, pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi.
    Na Pluijm anaamua kwenda Singida United baada ya kusitishiwa mkataba wa Ukurugenzi wa Ufundi wa Yanga wiki iliyopita.
    Pluijm akimkabidhi jezi kiungo Tafadzwa Kutinyu kutoka Chicken Inn Fcya Zimbabwe baada ya kusajili mkataba wa miaka miwili 

    Yanga ilimhamishia Pluijm kwenye Ukurugenzi wa Ufundi Novemba mwaka jana, baada ya kumleta Mzambia, George Lwandamina awe kocha Mkuu.
    Pluijm amefundisha Yanga kwa awamu mbili tangu mwaka 2014 alipoanza kwa kufanya kazi kwa nusu msimu, akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts kabla ya kwenda Uarabuni.
    Alikwenda Al Shoalah FC ya Saudi ya Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Marcio Maximo ambaye naye alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana. 
    Saudi Arabia ambako alikwenda na aliyekuwa Msaidizi wake, Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa – Pluijm  aliondoka baada ya kutofautiana na uongozi wa timu uliotaka kumsajilia wachezaji asiowataka.
    Kabla ya kuhamishiwa kwenye Ukurugenzi wa Ufundi, Pluijm aliiongoza Yanga katika jumla ya mechi 128, akishinda 80, sare 25 na kufungwa 23.
    Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 110 za tangu mwaka jana, alishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.
    Msimu uliopita ulikuwa mzuri zaidi kwake, akibeba mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
    Pluijm pia aliiwezesha Yanga kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria. Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
    Na kwa mafanikio hayo, haikuwa ajabu Pluijm akishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa msimu uliopita.
    Mapema wiki hii, Singida United ilimsajili kiungo Tafadzwa Kutinyu kutoka Chicken Inn Fc ya Zimbabwe kwa mkataba wa miaka miwili. 
    Singida United imerejea Ligi Kuu msimu huu baada ya msoto wa zaidi ya miaka 15 tangu ishuke Daraja.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PLUIJM ATUA SINGIDA UNITED NA KUSAJILI ‘MIDO’ MZIMBABWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top