• HABARI MPYA

  Tuesday, March 07, 2017

  MJERUMANI APEWA AMAVUBI, TAIFA STARS WAJIPANGE CHAN

  SHIRIKISHO la Soka Rwanda (FERWAFA) limeteua Mjerumani Antoine Hey kuwa kocha wake mpya wa timu ya taifa kwa mkataba wa miaka miwili.
  Hey amepiku Raoul Savoy wa Uswisi na Rui Aguas wa Ureno, alioingia nao fainali ya orodha ya mwisho ya watu watatu kuwania kurithi mikoba ya Johnny McKinstry aliyeacha kazi Agosti mwaka jana.
  “Kwa Hey, nafikiri tumefanya uteuzi mzuri, hususan tukizingatia tuna uhusiano na Ujerumani,” amesema Rais wa FERWAFA, Vincent Nzamwita.
  Mjerumani Antoine Hey ndiye kocha mpya wa timu ya taifa ya Rwanda kwa miaka miwili ijayo

  Kocha huyo mwenye umri wa miaka 46 anatarajiwa kutambulishwa siku chache zijazo. Hey ana uzoefu na soka ya Afrika kwa ngazi ya timu za taifa na hata klabu, kwani amewahi kufundisha Lesotho kati ya mwaka 2004 na 2006 kabla ya kuhamia Gambia na baadaye klabu ya US Monastir ya Tunisia mwaka 2007. 

  Pia amefanya kazi Liberia, Kenya na hivi karibuni El-Merreikh ya Sudan. Anaingia katika orodha ya makocha wa Kijerumani waliofanya kazi Amavubi, wengine wakiwa ni Otto Pfister aliyefundisha 1972 hadi 1976, Rudi Gutendorf kuanzia 1999 hadi 2000 na Michael Nees aliyepiga kazi 2006 hadi 2007.
  Ikumbukwe Rwanda itamenyana na Tanzania, Taifa Stars katika kuwania tiketi ya Fainali za Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) mwaka 2018 nchini Kenya.
  Hiyo ni itakuwa katika Raundi ya pili ya mchujo wa michuano hiyo inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee na Taifa Stars itaanzia nyumbani Dar es Salaam Julai 14, 15 na 16 mwaka huu kabla ya kuwafuata Amavubi Kigali kati ya Julai 21, 22 na 23.
  Mshindi wa jumla atamenyana na mshindi kati ya Uganda na ama Sudan Kusini au Somalia katika Raundi ya Tatu ya mchujo mechi ya kwanza ikichezwa kati ya Agosti 11, 12 na 13 na marudiano kati ya Agosti 18, 19 na 20, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MJERUMANI APEWA AMAVUBI, TAIFA STARS WAJIPANGE CHAN Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top