• HABARI MPYA

  Monday, March 13, 2017

  MAYANGA ATAJA STARS MPYA, JUMA ABDUL, YONDAN NA MWINYI MNGWALI NJE

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Mayanga ameita wachezaji 26 kwa ajili ya maandalizi maandalizi ya michezo ya kufuzu michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). 
  Katika kikosi hicho, Mayanga hajawajumuisha mabeki wa Yanga, Juma Abdul, Kevin Yondan, Mwinyi Hajji Mngwali na wa Azam, Aggrey Morris na David Mwantika.
  Kuhusu Mngwali na wachezaji wengine wa Zanzibar, Mayanga amesema hajawaita kwa sababu anasubiri maamuzi ya kikao cha Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Machi 16 kuhusu kuipa uanachama nchi hiyo.
  "Kama Zanziabr itapewa uanachama CAF, ina maana hatutaendelea kuchanganyika na Zanzibar, lakini kama ikikwama, basi nitawarudisha wachezaji wa Zanzibar, nimeacha nafasi nne kwa ajili hiyo," amesema. 
  Mayanga aliyetaja kikosi hicho asubuhi ya leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam - amewachukua washambuliaji chipukizi, Mbaraka Yussuf wa Kagera Sugar na Abdulrahman Juma wa Ruvu Shooting. 
  Kocha Salum Mayanga ameita wachezaji 26 Taifa Stars kwa maandalizi ya kufuzu CHAN na AFCON. Kulia ni Msemaji wa TFF, Alfred Lucas

  Kwa ujumla kikosi alichoteua Mayanga kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Azam), Deogratius Munishi ‘Dida’ (Yanga) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
  Mabeki; Shomary Kapombe (Azam), Hassan Kessy (Yanga), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba), Gardiel Michael (Azam), Andrew Vincent (Yanga), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba) na Erasto Nyoni (Azam FC).
  Viungo ni Himid Mao (Azam), Jonas Mkude (Simba), Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam), Said Ndemla (Simba), Frank Domayo (Azam), Muzamil Yassin (Simba), Simon Msuva (Yanga), Shiza Kichuya (Simba), Farid Mussa (DC Tennerife) na Hassan Kabunda (Mwadui FC).
  Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna, Sweden), Ibrahim Hajib (Simba), Mbarak Yussuf (Kagera Sugar) na Abdulrahman Mussa (Ruvu Shooting).
  Mayanga aliwasili ofisi za TFF kutaja kikosi akiwa ameongozana na Ofisa Habari, Alfred Lucas huku mvua ikinyesha

  Aidha, Mayanga ametaja benchi lake la Ufundi na Msaidizi wake atakuwa Patrick Mwangata ambaye pia kocha wa makipa, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa Ally Ruvu, Daktari Richard Yomba, Daktari wa Viungo, Gilbert Kigadya.
  Mayanga amesema timu hiyo itaingia kambini Machi 19 mjini Dar es Salaam na itacheza mechi mbili za kujipima nguvu.
  Mechi zote zitafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Botswana Machi 25 na Burundi Machi 28.
  Mechi hizo ni maandalizi ya michezo ya kufuzu michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). 
  Taifa Stars itaanza na Rwanda katika kuwania tiketi ya CHAN mwakani nchni Kenya na mechi ya kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kati ya Julai 14 na 16 kabla ya timu hizo kurudiana Uwanja wa Amahoro, Kigali kati ya Julai 21 na 23.
  Ikifanikiwa kuitoa Rwanda, Tanzania itamenyana na mshindi kati ya Uganda na ama Sudan Kusini au Somalia katika Raundi ya Tatu ya mchujo mechi ya kwanza ikichezwa kati ya Agosti 11, 12 na 13 na marudiano kati ya Agosti 18, 19 na 20, mwaka huu.
  Tanzania imewahi kushiriki mara moja tu fainali za CHAN, ambayo ilikuwa ni mwaka 2009 zikifanyika kwa mara ya kwanza kabia.
  Kwa upande wa AFCON, Taifa Stars imepangwa Kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho.
  Mshindi wa kila kundi atafuzu moja kwa moja AFCON ya 2019, wakati timu nyingine tatu zitakazomaliza nafasi ya pili na wastani mzuri zaidi ya nyingine zitafuzu kama washindi wa pili bora. 
  Tanzania imewahi kucheza mara moja tu fainali za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilitolewa hatua ya makundi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAYANGA ATAJA STARS MPYA, JUMA ABDUL, YONDAN NA MWINYI MNGWALI NJE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top