• HABARI MPYA

  Sunday, March 19, 2017

  MAVUGO AIPELEKA SIMBA NUSU FAINALI KOMBE LA TFF

  Na Mwandishi Wetu, ARUSHA
  BAO pekee la mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo limeipeleka Simba SC Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kuwalaza wenyeji, Madini FC 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ahmad Kikumbo wa Dodoma, aliyesaidiwa na Abdallah Mkomwa na Khalfan Sika, Mavugo alifunga bao hilo dakika ya 55 kwa kichwa baada ya kuufikia mpira wa juu uliomshinda beki wa Madini, Hamisi Hamisi.
  Laudit Mavugo ameifungia bao muhimu Simba SC leo Uwanja Sheikh Amri Abeid

  Hiyo ilifuatia dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza wenyeji wakicheza kwa kujilinda zaidi na kushambulia kwa kushitukiza, hivyo kuwadhibiti vigogo hao kutoka Dar es Salaam.
  Baada ya bao hilo, Madini wakafunguka na kuanza kucheza kwa kushambulia moja kwa moja kusaka bao la kusawazisha, jambo ambalo liliwafungulia njia Simba nao kufikisha mashambulizi lao kwa wenyeji wao. 
  Beki Hamisi Hamisi akaokoa bao la wazi dakika ya 69 baada ya kuzuia shuti la winga machachari wa Simba, Shiza Kichuya lililokuwa linaelekea nyavuni na kuondosha kwenye hatari.
  Simba SC inaungana na Mbao FC ya Mwanza iliyowatoa wenyeji, Kagera Sugar kwa mabao 2-1 jana Uwanja wa Kaitaba, Bukoba kwenda Nusu Fainali ya michuano hiyo ambayo mwaka jana walitolewa na Coastal Union ya Tanga katika Robo Fainali.
  Mechi nyingine mbili mbili za Robo Fainali kati ya Azam FC na Ndanda FC na Yanga SC na Prisons zitapangiwa tarehe.
  Kikosi cha Simba kilikuwa; Daniel Agyei, Janvier Besala Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Juuko Murshid, James Kotei, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin/Jonas Mkude dk58, Laudit Mavugo, Ibrahim  Hajib/Pastory Athanas dk70 na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Said Ndemla dk46.
  Madini FC; Ramadhani Chalamanda, Lazaro Constantine, Makiwa Feruzi, Hamisi Hamisi, Priscus Julius, Edward Eliau, Gibson Joseph, Shaaban Imamu, Athumani Dennis, Awesu Awesu/Rajab Mwaluko dk72 na Mohammed Athumani/Mohammed Athumani dk56. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAVUGO AIPELEKA SIMBA NUSU FAINALI KOMBE LA TFF Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top