• HABARI MPYA

    Monday, March 13, 2017

    MALINZI AWAPA MAAGIZO MAZITO MAKOCHA WAPYA, AMLILIA SIR GEORGE KAHAMA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amewazawadia makocha wapya 27 waliofuzu kozi ya ukocha kwamba kila mmoja mmoja atampa koni 20 na vizibao 22 kwa ajili ya mazoezi.
    Rais Malinzi alitoa ahadi hiyo wakati wa hafla ya kufunga kozi ya ukocha ngazi ya ‘Intermidiate’ kwa makocha waliohitimu. Rais Malinzi alialikwa na waratibu kuwa mgeni rasmi ambaye awali, alishangazwa kwa namna ilivyoratibiwa kwa kufuata miongozi ya TFF na CAF.
    Katika hotuba yake, Rais Malinzi aliwataka waamuzi hao kuzingatia weledi wakiwa ni mabalozi wa kupinga matumizi ya dawa za kulevya lakini zaidi wajiepushe kwa njia yoyote ile kupanga matokeo.
    Rais Malinzi alifurahishwa na idadi kubwa ya makocha waliohitimu kwani kabla walikuwa ni wachezaji wa timu kubwa na kongwe mbalimbali, “Hilo sasa linanisukuma kuwapa kila mmoja wenu koni 20 na bips (vizibao) 22,” alisema Rais Malinzi.
    Alitumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania kuwaombea dunia Rais wa Heshima wa TFF, Leodegar Chilla Tenga ambaye anawania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji wa FIFA kwa nchi zinazozungumza Kiingereza ambako anapambana na Kwesi wa Ghana.
    Pia katika mkutano huo Mkuu wa CAF utakaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia ukihusisha nchi 53 kati ya 54 wanachama wa CAF, pia watapiga kura kuichagua Zanzibar kuwa mwanachama kamili wa shirikisho hilo.
    Kozi hiyo iliendeshwa na Wilfred Kidao - Mkufunzi anayetambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), akisaidiwa na Manyika Peter aliyefundisha programu au mtaala kwa makocha wa makipa; Dk. Nassoro Ally Matunzya aliyewanoa makocha hao kuhusu tiba za wanamichezo/wanasoka na Mkufunzi wa muda mrefu wa soka, Hemed Mteza.
    Wahitimu wa kozi hiyo walikuwa Doris Malyaga ambaye ni Mwanamke pekee kati ya wanafunzi 27 walisoma kozi hiyo kwa kipindi cha siku 14 cha mwanzo wa mwaka. Doris ni mwanahabari za michezo aliyehudhuria kozi hiyo. Anaandikia gazeti la MwanaSPOTI linalotolewa na Kampuni ya Magazeti ya Mwananchi (MCL).
    Wengine ni nyota wa zamani wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ waliopata kuchezea klabu kongwe na kubwa nchini. Wanafunzi hao ni Boniface Pawasa, Fred Mbuna, Innocent Haule, Herry Morris, Ivo Mapunda, Nizar Khalfan na Mussa Hassan Mgosi.
    Wengine ni Omar Kapilima, Amosi Mgisa, Uhuru Mwambungu, Yussuf Macho, George Minja, Haruna Adolf, Selemani Omari, Ally Ruvu, Masoud Selemani, Haji Mustapha, Mhasham Khatib, Issa Ndunje, Salum Kapilima, Said Salum, Julio Elieza, Hassan Mwakami, Rajab Mponda, Ally Mbonde na Evod Mchemba.
    Wakati huo huo: Malinzi, ametuma rambirambi kwa familia ya marehemu Sir George Kahama aliyefariki dunia Jumapili akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
    Rais Malinzi amesema taifa limepoteza mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika kupigania maendeleo ya mpira wa miguu baada ya kupigania Uhuru ambao Watanzania leo wanajivunia amani.
    Pamoja na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki, Rais Malinzi Dkt Magufuli amewapa pole wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi, akisema ni kielelezo cha kiongozi aliyetukuka.
    “Kabla ya Uhuru Mzee wetu, Mzee Kahama alikuwa kiongozi shupavu na mzalendo, alama ambayo ametuachia sisi Watanzania leo hii tunajivunia amani,” alisema Rais Malinzi.
    Rais Malinzi ambaye katika vikao vyake vya jana hapa Dar es Salaam, alikuwa akitoa nafasi ya kumkumbuka Sir George, akisema msiba huo pia ni wa TFF kwa kuwa mmoja wa watoto wake, Joseph ni Mjumbe wa Mfuko wa Bodi ya Maendeleo ya Mpira wa Miguu wa TFF.
    Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI AWAPA MAAGIZO MAZITO MAKOCHA WAPYA, AMLILIA SIR GEORGE KAHAMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top