• HABARI MPYA

    Sunday, March 12, 2017

    KILA LA HERI AZAM FC, WATANDIKENI WASWAZI TUSONGE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    AZAM FC leo itaanza kampeni ya kusaka hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kumenyana na Mbabane Swallows ya Swaziland katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 32 Bora Uwanja wa Azam Complex kuanzia Saa 1.15 usiku.
    Azam FC itaingia kwenye mchezo huo wa raundi ya kwanza wa michuano hiyo ikiwa na morali kubwa baada ya kujikusanyia matokeo bora katika mechi walizocheza mwaka huu, huku ikionekana kuwa na safu ngumu ya ulinzi baada ya kuruhusu wavu wake kuguswa mara moja katika mechi 15 walizocheza mwaka huu.
    Mpaka sasa katika mechi saba zilizopita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Azam FC imefanikiwa kucheza bila wavu wake kutikiswa jambo ambalo limekuwa likizidi kuiongezea morali timu hiyo kadiri inavyozidi kucheza mechi zake.
    Hii itakuwa ni mara ya tano mfululizo kwa Azam FC kuingia kwenye changamoto ya michuano ya Afrika, ambapo hata mwaka huu katika malengo waliyojiwekea imeendelea kushikilia msimamo wake wa kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo.
    Katika mara hizo tano, ni mara mbili tu Azam FC imefanikiwa kuingia hatua ya 16 bora (2013, 2016), zote ikiwa kwenye kombe la Shirikisho Afrika ikiwemo na mwaka 2015 iliposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-2 katika raundi ya awali.
    Kuelekea mtanange huo unaosubiriwa na mashabiki wengi wa soka nchini, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, amesema wamejipanga kufanya vema kesho huku akidai kuwa moja ya mipango yao ni kuutumia vizuri mchezo huo wa kwanza kwa kupata ushindi mzuri.
    “Maandalizi tumefanya vizuri, wachezaji wako vizuri katika mazoezi na wanaari na wanataka kuhakikisha wanamaliza mechi hapa nyumbani, morali ya vijana iko juu hata kwa mazoezi wanaonekana wanaumoja, wanashikamana, wanajituma na wanataka kuhakikisha tunavuka raundi hiyo,” alisema.
    Alisema katika kuhakikisha wanavuka raundi hiyo, basi mechi hii ya kwanza ni muhimu kwao kwa kufanikisha ushindi ambao ni mzuri ambao utawarahisishia katika mechi ya marudiano itakayofanyika mjini Mbabane, Machi 19 mwaka huu.
    “Kama makocha, wachezaji na uongozi bado tuna mikakati ya kufika hatua ya robo fainali, na ndio maana kuna umoja mkubwa, tunachoomba mashabiki na wao kutusapoti katika hilo, unajua nao wanafasi fulani ya kutusaidia kwenye hilo kwa kuwajaza morali zaidi wachezaji ili kutupa ushindi,” alisema.

    Mbabane Swallows nayo ikoje?
    Mbabane Swallows iliyoanzishwa mwaka 1948 ikijulikana kwa jina , hii ni mara yao ya 10 kushiriki michuano ya Afrika, mara zote huko nyuma ikishiia raundi za awali, ambapo mafanikio makubwa ni kuishia raundi ya kwanza mara nne mfululizo zilizopita, ikiwa imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Mara ya mwisho mwaka juzi, ilitolewa na Zesco United ya Zambia kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 nyumbani kwao kabla ya kufungwa ugenini 1-0.
    Kihistoria katika michuano ya Afrika, hii ni mara ya pili kwa Mbabane kukutana na timu kutoka Tanzania, ambapo mwaka 1995 kwenye Kombe la CAF (ambalo kwa sasa linajulikana kama Kombe la Shirikisho Afrika) ilikutana na Malindi ya Zanzibar na kutolewa kwa jumla ya mabao 3-0, ikifungwa 2-0 ugenini na ikaloa nyumbani 1-0.
    Malindi iliandika historia mwaka huo baada ya kufika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kabla ya kutolewa na Etoile Sportive du Sahel kwa penalty 4-3 kufuatia kutoka sare ya jumla ya bao 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
    Kwa mujibu wa takwimu za Ligi Kuu ya Swaziland msimu huu, inaonyesha kuwa mpaka sasa Mbabane imecheza jumla ya mechi 16 na kupata ushindi wa mechi zote bila kufungwa wala kutoka sare, huku ikifungwa mchezo mmoja wa Kombe la Swazi Bank mabao 2-1 wikiendi iliyopita dhidi ya Matsapha United.
    Katika ligi hiyo mshambuliaji wake hatari, Sabelo Ndzinisa 'Sikhali', ndiye kinara wa ufungaji kwenye ligi akiwa na mabao 15 akifuatiwa na mshambuliaji mwingine wa timu hiyo Sandile Hlatjwako, aliyefunga 10.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI AZAM FC, WATANDIKENI WASWAZI TUSONGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top