• HABARI MPYA

    Thursday, March 02, 2017

    AFRICAN LYON: TUNATAFUTA NGUVU YA UWEKEZAJI KATIKA TIMU

    Na Mwandishi Wetu, DAE ES SALAAM
    MMILIKI wa African Lyon, Rahim Kangenzi ‘Zamunda’ amesema kwamba anatafuta nguvu ya uwekezaji ndani ya timu yake na si kuiuza moja kwa moja kama inavyofikiriwa.
    Hiyo inafuatia kuwapo taarifa kwamba GSM Limited iko mbioni kuinunua African Lyon, baada ya kushindwa kumilikishwa Maji Maji ya Songea.
    Leo mchana Bin Zubeiry Sports – Online iliandika kwamba mazungumzo kati ya uongozi wa GSM chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Ghalib Mohammed na African Lyon yanaendelea na inaelezwa yamefikia pazuri na wakati wowote dili hilo linawezwa kuwekwa wazi.
    Rahim Kangenzi ‘Zamunda’ amesema kwamba anatafuta nguvu ya uwekezaji ndani ya African Lyon

    “Tunatafuta nguvu ya uwekezaji ndani ya timu na si kuiuza kama inavyofikiriwa. GSM ni watu ambao kwa sasa wanatusaidia sana na milango iko wazi mtu yeyote anayetaka kuja kununua hisa,”amesema.
    Zamunda aliinunua Lyon mwaka 2010 kwa Mohammed Dewji, ambaye naye aliinunua mwaka 2007 kwa wafanyabiashara wa soko la Mbagala, enzi hizo ikiitwa Mbagala Market.
    Na GSM wanataka kuinunua Lyon baada ya mpango wa kutaka kumilikishwa Maji Maji kushindikana kutokana na wanachama wa klabu hiyo kukataa. Kwa sasa GSM ni wafadhili wa Maji Maji ya Ruvuma, mkoa ambao anatokea Ghalib.
    Kwa kuwa GSM sasa wanaamua kuwekeza kwenye soka, wakiwa na mpango wa kumiliki klabu kubwa hapa nyumbani mithili ya Azam FC, yenye Uwanja wake, akademi na kujiendesha kisasa – wanalazimika kununua timu nyingine.
    “Mazungumzo na Lyon yanaendelea, wakati wowote mipango ikikaa sawa itatangazwa hadharani, kwa sasa bado,”kimesema chanzo kutoka GSM.  
    Habari zaidi zinasema kwamba GSM wanasubiri kuona kama African Lyon itabaki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ndiyo waweze kufanya biashara hiyo.
    Kwa sasa Lyon ipo nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu ya timu 16 ikiwa na pointi 22 za mechi 23 na bado ina kibarua cha kupigana kuhakikisha inakuwa nje ya timu ya timu tatu za chini zitakazoshuka Daraja kuzipisha Lipuli ya Iringa, Mji ya Njombe na Singida United ya Singida zilizopanda kuelekea msimu ujao.     
    Iko juu ya Toto African ya Mwanza, Maji Maji zenye pointi 22 za mechi 23 pia kila moja na JKT Ruvu yenye pointi 20 za mechi 24. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AFRICAN LYON: TUNATAFUTA NGUVU YA UWEKEZAJI KATIKA TIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top