• HABARI MPYA

    Thursday, February 02, 2017

    FIFA YAITAKA YANGA KUMLIPA BRANDTS MILIONI 20 ZAKE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Kimataifa (FIFA), limeitaka Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam kulipa mara moja deni la aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ernst Wilhelmus Johannes Brandts - Raia wa Uholanzi waliyevunja naye mkataba miaka miwili iliyopita.
    Klabu ya Yanga imetakiwa kulipa dola 11,000 za Marekani kama ambavyo iliamriwa Juni 30, 2015 na Kamati ya Hadhi ya Wachezaji ya FIFA.
    Kwa kuchelewa kulipa fedha hizo tangu Juni, 2015, Yanga imeamriwa pia ilipe fidia ya asilimia tano ya deni halisi.
    Yanga wametakiwa kulipa fedha hizo na kutuma nakala ya malipo hayo, kabla ya shauri hilo halijapelekwa Kamati ya Nidhamu.
    Kocha Mholanzi, Ernie Brandts enzi zake akifanya kazi Yanga SC

    Kutolipa deni hilo kwa wakati, imetafsiriwa kwamba Yanga imevunja Kanuni ya 64 inayozungumzia Nidhamu katika FIFA yaani FDC (FIFA Disciplinary Committee).
    Yanga inakabiliwa adhabu za kupigwa faini zaidi ya awali, kukatwa pointi katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoendelea kwa sasa au kushushwa daraja.
    Kamati hiyo ya Nidhamu inatarajiwa kukutana wakati wowote wiki ijayo na suala la Nidhamu ya Yanga litakuwa ajenda ili kama hawakulipa, watachukua hatua kama adhabu zinavyojieleza hapo juu
    TFF imeagizwa haraka kufuatilia suala la deni hilo katika klabu ya Yanga na kurudisha majibu FIFA. TFF kupitia Katibu Mkuu, imeagizwa kupeleka barua ya FIFA katika Makao makuu ya Klabu hiyo, yaliyoko kwenye makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam.
    "TFF tumeliweka wazi suala hilo kama ‘Tahadhari kabla ya hatari’, kwani tungeweza kufanya mawasiliano kati ya shirikisho (TFF) na klabu (Young Africans) kwa siri tu, lakini ikitokea huko mbele klabu inakutana na adhabu mojawapo, lawama hushuka TFF kwa madai kwamba tumekalia taarifa muhimu ya kuchukuliwa hatua haraka,"imesema taarifa ya TFF leo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FIFA YAITAKA YANGA KUMLIPA BRANDTS MILIONI 20 ZAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top