• HABARI MPYA

  Friday, February 03, 2017

  YANGA SC KULIPA KISASI KWA STAND UNITED LEO?

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja tu kupigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mabingwa watetezi, Yanga SC watakuwa wenyeji wa Stand United ya Shinyanga katikaa mchezo unaotarajiwa kuanza Saa 10:30 na kurushwa moja kwa moja na Azam TV kama kawaida.
  Mchezo huo ni muhimu mara mbili, kwa Yanga SC, kwanza kuwania pointi tatu ili kujiweka sawa katika kampeni zake za kutetea taji na pili kulipa kisasi cha kufungwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza.
  Septemba 25, mwaka jana Stand United walitumia vizuri Uwanja wa nyumbani, Kambarage mjini Shinyanga kuifunga 1-0 Yanga, bao pekee la Pastory Athanas ambaye amehamia Simba Desemba.
  Yanga walifungwa mechi hiyo wakati wakiwa chini ya kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi na nafasi yake imechukuliwa na Mzambia, George Lwandamina.
  Kwa maana hiyo, chini ya Lwandamina leo Yanga itakuwa na jukumu moja tu la kulipa kisasi kwa Stand United, inayofundishwa na mzalendo, Athumani Bilal baada ya kuondoka kwa Mfaransa, Patrick Liewig.
  Yanga na Stand United zinakutana leo zote zikitoka kuifunga Mwadui FC 2-0 katika mechi zao zilizopita, jambo ambalo linaashiria timu zote zina ubavu sawa na leo shughuli itakuwa pevu Uwanja wa Taifa.
  Kocha wa zamani wa Zesco Unite ya Zambia, George Lwandamina hatarijiwi kuwa na mabadiliko makubwa kikosini mwake kutokaa kile kikosi kilichofunga Mwadui FC 2-0 Jumapili Uwanja wa Taifa.
  Ingawa anaweza akamuanzisha kiungo mshambuliaji, Mzambia mwenzake, Obrey Chirwa aliyetokwa benchi Jumapili na kwenda kufunga mabao yote mawili ndani dakika 20 za mwisho.
  Lakini Lwandamina ataendelea kuwakoa beki Mtogo, Vincent Bossou na mshambulaiji Mzimbabwe Donald Ngoma ambao hawajarejea kutoka kwao.
  Hakuna shaka katika safu ya ulinzi ataendelea kuwapanga wazoefu, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan baada ya wote kumlinda vizuri kipa Deo Munishi ‘Dida’ Jumapili wakisaidiana na Juma Abdul kulia na Mwinyi Hajji Mngwali kushoto.
  Lwandamina anaweza kumuanzisha tena kiungo Mzambia mwenzake, Justin Zulu baada ya kucheza vizuri Jumapili, sambamba na kiungo mwenye mambo mengi, Mnyarwanda Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima pale mbele kuichezesha timu.
  Simo Msuva anaweza kurudi kwenye wingi ya kulia sawa na kiungo Mzimbabwe Thabani Kamusoko na Mrundi Amissi Tambwe akaanzishwa tena kama mshambuliaji pekee, lakini haitakuwa ajabu Deus Kaseke akimpisha Chirwa leo.    
  Ikumbukwe Yanga SC ndiyo wanaongoza Ligi Kuu kwa sasa kwa pointi zao 46 baada ya kucheza mechi 20, wakifuatiwa na Simba SC wenye pointi 45 za mechi 20 pia, wakati Kagera Sugar yenye pointi 37 za mechi 21 ni ya tatu, Azam yenye pointi 34 za mechi 20 ya nne na Mtibwa Sugae yenye pointi 31 za mechi 20 ni ya tano. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC KULIPA KISASI KWA STAND UNITED LEO? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top