• HABARI MPYA

  Sunday, February 05, 2017

  YANGA KWENDA COMORO IJUMAA MECHI YA KWANZA LIGI YA MABINGWA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC inatarajiwa kuondoka nchini Ijumaa ijayo kwenda Comoro kwa ajili ya mchezo wa mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Ngaya Club.
  Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa aliiambia Bin Zubeiry Sports - Online jana kwamba wanatarajia kuondoka siku mbili kabla ya mechi hiyo ya kwanza ya ugenini.
  “Taarifa rasmi za safari tunaweza kutoa Jumatatu, baada ya kukutana na benchi la Ufundi na kuzungumza nao, ili na wao watupe mipango yao,”alisema Mkwasa, ambaye pia kitaaluma ni kocha wa daraja la juu.
  Baada ya kuifunga Stand United juzi mabao 4-0 katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga watakuwa na maandalizi ya wiki nzima kuelekea mchezo wa Comoro.
  Na huu ni msimu wa pili mfululizo Yanga inaanza na timu za Comoro baada ya mwaka jana pia kuitoa Cercle de Joachim kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Katika Raundi ya Kwanza Yanga iliitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 ugenini na kutoa sare ya 1-1 nyumbani.
  Mbio za Yanga katika Ligi ya Mabingwa ziliishia Raundi ya Pili inayohusisha timu 16, baada ya kutolewa na wababe wao wa kihistoria, Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 3-2, ikitoa sare ya 1-1 Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 2-1 Alexandria ndani ya dakika 120 baada ya mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
  Yanga ikaangukia kwenye kapu la kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako iliitoa Sagrada Esperanca ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 Dar es Salaam Mei 7 na kufungwa 1-0 Mei 18 katika mchezo wa marudiano Esperanca, Angola.
  Katika mechi za makundi, Yanga ilishinda mchezo mmoja tu dhidi ya MO Bejaia ya Algeria Agosti 13, 2016 na kutoa sare moja na Medeama ya Ghana Julai 16, 2016 zote uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mechi nyingine ilifungwa 1-0 Bejaia Juni 20 ugenini, ikafungwa 1-0 nyumbani na TP Mazembe ya DRC Juni 28, ikafungwa 3-1 na Medeama Julai 26 ugenini kabla ya kumaliza kwakipigo cha 3-1 mbele ya Mazembe Agosti 23 mwaka jana Lubumbashi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KWENDA COMORO IJUMAA MECHI YA KWANZA LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top