• HABARI MPYA

    Sunday, February 05, 2017

    WATANZANIA WANATAKA KUSIKIA PROGRAMU YA MAANDALIZI YA SERENGETI BOYS

    WATANZANIA wataishuhudia tena timu yao ya taifa ikicheza fainali za Afrika Aprili mwaka huu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2009.
    Timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars ilikuwa ya mwisho kucheza fainali za Afrika mwaka 2009 ilipocheza Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza Ligi za nchini mwao pekee. 
    Hiyo ilikuwa ni nchini Ivory Coast ambako ilitolewa hatua ya makundi – na Aprili mwaka huu timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys itacheza fainali nyingine. 
    Serengeti imerejeshwa kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo baada ya kushinda rufaa yake dhidi ya Kongo Brazzaville iliyotumia mchezaji aliyezidi umri.
    Mwanzoni mwa mwezi uliopita, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliwapa siku 10 Shirikisho la Soka Kongo (FECOFOOT) kumuwasilisha mchezaji Langa Lesse Bercy mjini Libreville, Gabon afanyiwe vipimo vya MRI ili kuthibitisha umri wake kama anaruhusiwa kucheza mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17, lakini wameshindwa kufanya hivyo.
    Na hiyo ilikuwa mara ya tatu, FECOFOOT wanashindwa kumpeleka Langa Lesse Bercy akafanyiwe vipimo baada ya kushindwa kufany hivyo awali mara mbili mjini Cairo, Misri kwa vipimo.
    Fainali za U-17 Afrika ilikuwa zifanyike nchini Madagascar kuanzia Aprili mwaka huu, lakini mwezi uliopita CAF iliivua uenyeji na kutoa muda hadi Januari 30 mwaka huu nchi nyingine kujitokeza kuomba uenyeji kabla ya juzi kuiteua Gabon kuandaa fainali hizo.
    Kongo Brazaville iliitoa Tanzania katika hatua ya mwisho ya mchujo kwa jumla ya mabo 3-2, baada ya sare ya 2-2 Dar es Salaam na ushindi wa 1-0 nyumbani kwao.
    Lakini kitendo cha kutumia mchezaji aliyezidi umri kinawagharimu na kuondolewa kwenye mashindano, Tanzania wakichukua nafasi hiyo.
    Adhabu kama hii waliwahi kuipata Tanzania baada ya kufuzu fainali za U-17 Gambia mwaka 2005, lakini ndani yake wakawa na mchezaji aliyezidi umri, Nurdin Bakari. 
    Na kwa fainali za mwaka huu zitakazofanyika Gabon, Serengeti Boys imepangwa Kundi B pamoja na Angola, Mali na Niger.
    Katika makundi yaliyotolewa jana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wenyeji Gabon watakuwa Kundi A pamoja na Guinea, Cameroon na Ghana na michuano hiyo itaanza Aprili 2 mwaka huu.
    Jioni ya Ijumaa baada ya kuvuja kwa habari za Serengeti kushind rufaa, wadau mbalimbali wa michezo, wakiwemo viongozi wa Serikali walionyesha hisia zao.
    Zilikuwa hisia za furaha baada ya nafasi hiyo, iliyotokana na juhudi binafsi za TFF, chini ya Rais wake, Jamal Malinzi kupigania rufaa yake hadi dakika ya mwisho.
    Na sasa kihistoria hizi zitakuwa fainali za tatu za michuano mikubwa Tanzania inashiriki baada ya awali kabisa Taifa Stars kucheza Kombe la Mataifa Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria.
    Kwetu Tanzania nafasi ya kwenda Gabon imekuja kwa bahati, kwani ukiachilia mbali tulikuwa tumekwishatolewa, lakini hata mwenendo wa rufaa ulikuwa umekwishaanza kukatisha tamaa.
    Na tayari kulikuwa kuna minong’ono kwamba ni vigumu kushinda rufaa dhidi ya nchi inayozungumza Kifaransa, kama lugha ya taifa kwa madai hao ni maswahiba wa Rais wa CAF, Issa Hayatou.
    Lakini hatimaye haki imetendeka na Serengeti imerejeshwa kwenye mashindano hayo.
    Tupo mwanzoni mwa Februari 2017 na fainali za U-17 Gabon zitafanyika mapema Aprili, tuna wastani wa miezi miwili hapa katikati.
    Lugha ambayo itapendeza masikioni mwa Watanzania kwa sasa, ni kuhusu maandalizi ya timu hiyo kabla ya michuano hiyo.
    U-20 ya Zambia ilikuwa Hispania kwa wiki moja kucheza mechi za kujipima nguvu kujiandaa na fainali za U-20 Afrika ambazo wao baadaye watakuwa wenyeji baadaye mwaka huu.
    Juhudi za TFF katika kuijengea uwezo zaidi timu hiyo zinafahamika na imeshuhudiwa katika maandalizi yake ya mechi hizo za kufuzu ikienda kucheza mechi za kujipima hadi Asia.
    Kwa sasa lugha inayopendeza kusikia masikioni mwa Watanzania ni kuhusu maandalizi ya Serengeti Boys kuelekea fainali za Afrika Gabon.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WATANZANIA WANATAKA KUSIKIA PROGRAMU YA MAANDALIZI YA SERENGETI BOYS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top