• HABARI MPYA

  Monday, February 13, 2017

  WACHEZAJI SERENGETI BOYS WAPIMWA KUHAKIKIWA UMRI MUHIMBILI

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  ZOEZI la kuhakiki umri kwa wachezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys limekamilika salama chini ya usimamizi wa madaktari wa hospitali ya Taifa Muhimbili.                    
  Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Alfred Lucas ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba zoezi hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki hospitalini hapo na lilikwenda vizuri.
  “Na TFF imejiridhisha ipasavyo na umri wa wachezaji ambao sasa wanajiandaa kwa ajili ya fainali za Afrika kwa vijana wenye umri nchini ya miaka 17 zitakazofanyika Gabon Mei mwaka huu,”alisema Lucas.
  Wachezaji wa Serengeti Boys wakiwa jukwaani Uwanja wa Taifa Jumamosi kufuatilia mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Simba na Prisons 

  Serengeti Boys imepangwa Kundi B pamoja na Angola, Mali na Niger katika fainali za vijana chini ya umri wa miaka (AFCON U-17) Mei mwaka huu Gabon.
  Wenyeji Gabon watakuwa Kundi A pamoja na Guinea, Cameroon na Ghana na michuano hiyo itaanza Aprili 2 mwaka huu.
  Tanzania imerejeshwa kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo baada ya kushinda rufaa yake dhidi ya Kongo Brazzaville iliyotumia mchezaji aliyezidi umri.
  Mapema Januari Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliwapa siku 10 Shirikisho la Soka Kongo (FECOFOOT) kumuwasilisha mchezaji Langa Lesse Bercy mjini Libreville, Gabon afanyiwe vipimo vya MRI ili kuthibitisha umri wake kama anaruhusiwa kucheza mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17, lakini wameshindwa kufanya hivyo.
  Na hiyo ilikuwa mara ya tatu, FECOFOOT wanashindwa kumpeleka Langa Lesse Bercy akafanyiwe vipimo baada ya kushindwa kufanya hivyo awali mara mbili mjini Cairo, Misri kwa vipimo.
  Fainali za U-17 Afrika ilikuwa zifanyike nchini Madagascar kuanzia Aprili mwaka huu, lakini Januari CAF iliivua uenyeji na kutoa muda hadi Januari 30 mwaka huu nchi nyingine kujitokeza kuomba uenyeji kabla ya kuiteua Gabon kuandaa fainali hizo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WACHEZAJI SERENGETI BOYS WAPIMWA KUHAKIKIWA UMRI MUHIMBILI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top