• HABARI MPYA

    Wednesday, February 01, 2017

    ULIMWENGU ATOA PASI YA BAO, TIMU YAKE YATOA SARE HISPANIA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu jana ametoa pasi ya bao timu yake, AFC Eskilstuna ikipata sare ya 1-1 na Elfsborg zote za Ligi Kuu ya Sweden katika mchezo wa kirafiki nchini Hispania.
    Katika mchezo huo uliofanyika mjini Barcelona, Ulimwengu aliyejiunga na klabu hiyo mwishoni mwa Januari, alimsetia mshambuliaji wa Nigeria, Chidi Dauda Omeje kufunga bao hilo la  AFC Eskilstuna.
    Akizungimza na Bin Zubeiry Sports – Online jana kwa simu kutoka Hispania, Ulimwengu alisema kwamba anamshukuru Mungu ameanza vizuri katika timu yake mpya.
    Thomas Ulimwengu jana ametoa pasi ya bao timu yake, AFC Eskilstuna ikipata sare ya 1-1 na Elfsborg  
    “Leo (jana) tumecheza mechi ya kirafiki tumetoa sare ya 1-1 na mimi ndiye nimetoa pasi ya bao letu,”alisema mchezaji huyo aliyekaribia kusajiliwa Yanga mwaka 2012 akitokea Moro United, lakini akachagua kwenda AFC Eskilstuna, ambayo baadaye ilimuuza TP Mazembe.
    Kwa wiki nzima sasa, Ulimwengu yuko Hispania na klabu yake hiyo mpya, AFC Eskilstuna kwa maandalizi ya Ligi Kuu ya Sweden. 
    Ulimwengu amesaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, ambayo awali ilikuwa inajulikana kama FC Cafe Opera na Vasby United akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi 2011 TP Mazembe alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
    Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
    Ulimwengu anajivunia kushinda mataji makubwa akiwa na  Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ULIMWENGU ATOA PASI YA BAO, TIMU YAKE YATOA SARE HISPANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top