• HABARI MPYA

  Friday, February 17, 2017

  TFF YAWAONYA YANGA KUTOBEBA MABANGO YA KUIKASHIFU SERIKALI KESHO

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limewatahadharisha wanachama na wapenzi wa klabu ya Yanga, kutobeba mabango ya kukashifu Serikali wala kiongozi yeyote wa nchi kesho wakati wa mchezo wa marudiano na Ngaya Club de Mde ya Comoro.
  Yanga watakuwa wenyeji wa Ngaya katika mchezo wa marudiano Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na inahofiwa mashabiki wake wanaweza kubeba mabango ya kuwakashifu viongozi au Serikali, kufuatia Mwenyekiti wao, Yussuf Manji kushikikiwa na jeshi la Polisi kwa wiki moja.
  Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema jana kwamba wanawaonya mashabiki wa soka nchini waliopanga kuleta vurugu na kuonyesha viashiria vya kukashifu viongozi wa soka na Serikali katika mchezo wa wa kesho na wa Februari 25 dhidi ya Simba, wasithubutu.  
  Bonge kesho uende Taifa kistaarabu, usibebe bango wala kutukana 

  Lucas amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayethubutu kufanya kitu cha namna hiyo na kwamba kutakuwa na ulinzi mkali kesho Uwanja wa Taifa kwa ajili hiyo.
  Manji aliachiwa kwa dhamana jana mchana baada ya kusomewa shitaka la tuhuma za kutumia dawa za kulevya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
  Baada ya kusoma shitaka hilo, Hakimu Cyprian Mseha alimtaka mtuhumiwa huyo kufika mahakamani hapo Machi 16 kwa mwendelezo wa kesi hiyo.
  Manji aliwasili mahakamani chini ya ulinzi wa Polisi, akitokea kituo kikuu cha Polisi, Dar es Salaam alikuwa amewekwa rumande tangu Alhamisi.
  Hata hivyo, Jumamosi mchana Manji alipelekwa hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar es Salaam baada ya hali yake kubadilika na kuwa mbaya ikiwelezwa anasumbuliwa na matatizo ya moyo.
  Taarifa zilisema Manji alifanyiwa upasuaji mdogo na kurejeshwa Polisi jana, kabla ya jana kupandishwa kizimbani. 
  Manji aliwekwa rumande baada ya kujisalimisha mwenyewe kituo kikuu cha Polisi Alhamisi iliyopita, baada ya kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika orodha ya watu 65 wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
  Japokuwa Manji na wengine wote 64 waliotajwa walitakiwa kuripoti Polisi Ijumaa, lakini yeye alijipeleka mwenyewe Alhamisi pamoja na Askofu Gwajima, ambaye aliachiwa baada ya siku mbili.
  Na wakati tuhuma zake zikibadilika kutoka kwenye kushukiwa kuuza hadi kudaiwa anatumia dawa za kulevya, Manji pia anakabiliwa na shitaka lingine kupitia kampuni yake ya Quality Group Limited, kuajiri wageni bila vibali vya kufanya kazi nchini.
  Ofisa wa Idara ya Uhamiaji Dar es Salaam, John Msumule, alisema juzi kwamba Manji anatakiwa kufika ofisini hapo kujibu mashitaka ya kuajiri watu 25, ambao hawana vibali vya kufanya kazi nchini. 
  Msumule alisema ilikuwa wamkamate Manji Jumatatu wiki hii, lakini wakaambiwa amelazwa hospitali, hivyo wameacha maagizo akitoka hospitalini aripoti mwenyewe Ofisi ya Uhamiaji makao makuu Dar es Salaam.
  Msumule alisema kwamba walifanikiwa kukamata pasipoti 126 zenye makosa Jumamosi na kati ya hizo, 25 zilikuwa za waajiriwa ambao hawana vibali.
  Kiingilio cha chini katika mchezo wa kesho kitakuwa Sh. 3,000 Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, VIP A Sh 20,000, VIP B Sh 10,000 na VIP C Sh 10,000.
  Mechi hiyo itachezeshwa na marefa kutoka Uganda ambao ni Alex Muhabi Nsulumbi atayekapuliza filimbi uwanjani, akisaidiwa na washika vibendera Ronald Kakenya na Lee Okello.
  Refa wa Akiba atakuwa Brian Nsubuga Miro huku Kamishna akitokea Afrika Kusini ambaye ni Monnyenyone Lucas Nhlapo.
  Yanga ilishinda mabao 5-1 katika mchezo wa kwanza Jumapili mjini Moroni Comoro na wanatarajiwa kuwa na mteremko katika mchezo huo wa marudiano.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF YAWAONYA YANGA KUTOBEBA MABANGO YA KUIKASHIFU SERIKALI KESHO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top