• HABARI MPYA

  Friday, February 17, 2017

  TFF YAHANI MISIBA YA GEOFFREY BONNY NA MBAGA WA GREEN WARRIORS

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mbeya kutokana na kifo cha mchezaji wa zamani Tanzania Prisons, Yanga SC na timu ya taifa, Taifa Stars, Geoffrey Bonny.
  Taarifa kutoka Mbeya, zilizothibitishwa na uongozi wa Mkoa zinasema kwamba mchezaji huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia leo Ijumaa Februari 17, 2017 kwenye Hospitali ya Wilaya ya Rungwe.
  TFF itawakilishwa na Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya, Seleiman Haroub ambaye kwa sasa atashirikiana na familia kufanya taratibu za mazishi ambayo taarifa zaidi zitatangazwa baadaye mara baada ya vikao vya uamuzi.
  Geoffrey Bonny amefariki dunia usiku wa kuamkia leo mjini Mbeya

  Katika salamu zake za rambirambi, TFF imewataka ndugu wa marehemu kuwa na uvumilivu kwa kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito kwa Bonny ambaye nyota yake iling’ara zaidi wakati Taifa Stars inafundishwa na Mbrazil Marcio Maximo. 
  Katika hatua nyingine, TFF imesema pia imepokea kwa masikito taarifa ya kifo cha Nahodha wa timu ya 94 Green Warriors, Ikongo Julius Mbaga aliyefariki dunia leo alfajiri (Februari 17, 2017) kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo alikuwa amelazwa.
  Mchezaji huyo alijeruhiwa kwenye ajali ya gari ya timu yake iliyotokea Februari 13, 2017 Ihumwa mkoani Dodoma wakati ikiwa njiani kwenda Shinyanga kucheza mechi ya Ligi Daraja la Pili (SDL) dhidi ya Bulyanhulu FC.
  Taratibu za mazishi ya Marehemu ambaye mwili wake umehamishiwa Hospitali Kuu ya Jeshi (GMH) ya Lugalo jijini Dar es Salaam zinafanywa na familia yake kwa kushirikiana na klabu ya 94 Green Warriors. Taarifa rasmi za mazishi zitatolewa baadaye.
  TFF imetuma salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu, klabu ya 94 Green Warriors na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na uvumilivu kwa kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
  Kwa Msiba huu, Rais wa TFF Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa 94 Green Warriors, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huo mkubwa wa mpendwa wao. Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF YAHANI MISIBA YA GEOFFREY BONNY NA MBAGA WA GREEN WARRIORS Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top