• HABARI MPYA

  Friday, February 17, 2017

  SIMBA WAINGIA KAMBINI ZANZIBAR, MKUDE AWAWEKEA NADHIRI YANGA

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imekwenda leo kambini visiwani Zanzibar kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu, Yanga Jumamosi ya wiki ijayo, huku Nahodha Jonas Gerald Mkude akisema watashinda mechi hiyo. 
  Simba watakutana na watani wa jadi, Yanga Februari 25, mwaka huu katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na leo wameondoka kwa boti kwenda Zanzibar kwa kambi ya wiki moja.
  Mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu dhidi ya Yanga, Simba iliweka kambi Chuo cha Biblia, Bigwa mkoani Morogoro na baada ya kufungwa 2-0 na kutoa sare ya 1-1 sasa wanarejea Zanzibar.
  Kocha Joseph Omog (kulia) akizungumza na Msaidizi wake, Jackson Mayanja wakati wa safari ya Zanzibar leo

  Nahodha wa Simba, Jonas Gerald Mkude alisema jana kwamba hadi sasa wako vizuri kuelekea mchezo huo wa Februari 25.
  “Yanga ni timu kama timu nyingine, wao wanajiandaa na sisi tunajiandaa na wachezaji wote wako vizuri na dakika 90 ndizo zitakazoongea,”alisema.
  Simba inakwenda kambini Zanzibar siku moja baada ya kutinga Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) kufuatia kuifunga 1-0 African Lyon jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, bao pekee la Laudit Mavugo.
  Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Burundi, alifunga bao hilo dakika ya 57 baada ya kumzidi maarifa beki wa Lyon, Hassan Isihaka na kufumua shuti dhaifu lililompita kipa Mcameroon, Rostand Youthe kufuatia pasi ya mshambuliaji Ibrahim Hajib.  
  Nahodha wa Simba, Jonas Gerald Mkude amesema watawafunga Yanga Februari 25 

  Kikosi cha Simba kichoingia kambini leo kinaundwa na makipa; Daniel Agyei, Peter Manyika na Dennis Richard.
  Mabeki Janvier Bokungu, Hamad Juma, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Vincent Costa, Novaty Lufunga na Method Mwanjali.
  Viungo ni Jonas Mkude, James Kotei, Said Ndemla, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Muzamil Yassin, Mwinyi Kazimoto, Shiza Kichuya na Jamal Mnyate. 
  Washambuliaji ni Laudit Mavugo, Pastory Athanas, Ibrahim Ajibu, Hijja Ugando na Juma Luizio.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA WAINGIA KAMBINI ZANZIBAR, MKUDE AWAWEKEA NADHIRI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top