• HABARI MPYA

  Saturday, February 04, 2017

  SAMATTA AWATOA HOFU KRC GENK JUU YA MAUMIVU YAKE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba maumivu ya mgongo aliyoyapata Februari 1, mwaka huu hayatamuweka nje kwa muda mrefu, sana wiki moja tu. 
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kutoka Genk, Samatta alisema kwamba kwa sasa anaendelea vizuri na anatarajia wiki ijayo ataanza mazoezi.
  “Yalikuwa ni maumivu kidogo, ambayo sana nitakaa nje kwa wiki moja. Itategemea na jinsi nitakavyokuwa napata ahueni,”alisema.
  Mbwana Samatta amesema kwamba anatarajia kurejea uwanjani wiki ijayo baada ya kupona maumivu ya mgongo 

  Usiku wa Februari 1, Samatta alicheza kwa dakika 23 tu kabla ya kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo akiiacha timu yake, KRC Genk ikifungwa 1-0 na KV Oostende Uwanja Luminus Arena, Genk katika mchezo wa Kombe la Ubelgiji na kutolewa.
  Samatta aliumia dakika ya 23 na kulazimika kumpisha Mspaniola Jose Naranjo ambaye alikwenda kukosa penalti na bao la Mzimbabwe, Knowledge Musona dakika ya nane likaimaliza Genk.
  Huo ni mchezo wa pili mfululizo KRC Genk inapoteza, baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita pia kuchapwa 1-0 na KV Mechelen katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji. 
  Siku hiyo Samatta alicheza kwa dakika zote 90 jana Uwanja wa ugenini wa AFAS Achter de Kazerne mjini Mechelen na bao pekee la beki Mbelgiji, Seth De Witte dakika ya 89 likawapa wenyeji ushindi wa 1-0.
  Tayari Samatta amecheza mechi ya 40 tangu asajiliwe Genk Januari mwaka jana, 18 msimu uliopita na 22 msimu huu na kati ya hizo, ni michezo 21 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na 10 msimu huu.
  Mechi 19 kati ya hizo alitokea benchi, nane msimu uliopita na 11 msimu huu, wakati 10 hakumaliza baada ya kutolewa, sita msimu uliopita na nne msimu huu huku akiwa amefunga jumla ya mabao 11, matano msimu huu na sita msimu uliopita.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA AWATOA HOFU KRC GENK JUU YA MAUMIVU YAKE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top