• HABARI MPYA

  Thursday, February 16, 2017

  KUZIONA YANGA NA NGAYA CLUB SH 3,000

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KIINGILIO cha chini katika mchezo wa marudiano Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya wenyeji, Yanga SC na Ngaya Club de Mde ya Comoro kitakuwa Sh. 3,000 Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa leo ametaja viingilio vya mchezo huo katika Mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam. 
  Mkwasa, Nahodha na kocha wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, alisema eneo la CIP A kiingilio kitakuwa Sh 20,000, VIP B Sh 10,000 na VIP C Sh 10,000.
  Mechi hiyo itachezeshwa na marefa kutoka Uganda ambao ni Alex Muhabi Nsulumbi atayekapuliza filimbi uwanjani, akisaidiwa na washika vibendera Ronald Kakenya na Lee Okello.
  Refa wa Akiba atakuwa Brian Nsubuga Miro huku Kamishna akitokea Afrika Kusini ambaye ni Monnyenyone Lucas Nhlapo.
  Yanga ilishinda mabao 5-1 katika mchezo wa kwanza Jumapili mjini Moroni Comoro na wanatarajiwa kuwa na mteremko katika mchezo huo wa marudiano.
  Kocha Msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi akiuzungumzia mchezo huo amesema wanajivunia ushindi mnono walioupata ugenini, kwani ni hazina tosha kwao.
  “Lakini tunatambua umuimu wa mchezo wetu wa marejeano, ambao utafanyika siku ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, kikubwa tunawaomba mashabiki wetu na wanamichezo wajitokeze kwa wingi kuipa sapoti timu yao,”alisema.
  Katika mchezo huo, Yanga itawakosa wachezaji wake nyota watatu, kiungo Haruna Niyonzima anayesumbuliwa na Malaria na washambuliaji Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao ni majeruhi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KUZIONA YANGA NA NGAYA CLUB SH 3,000 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top